
Serikali imetangaza kuwa
kiwango cha chini cha taaluma anayopaswa kuwa nayo mwandishi wa habari kuwa ni
'Diploma ya Uandishi wa Habari' kwa mujibu wa kanuni za sheria mpya ya hunda za
habari zilizokamilika utungaji wake hivi karibuni.
Akizungumza
na wana habari leo mjini Dodoma, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
, Nape Nnauye (Pichani) amesema kuwa kanuni zimeshaundwa na zimechapishwa kwenye gazeti
la serikali tangu Februari 3 mwaka huu baada ya kupokea maoni ya wadau
mbalimbali.
"Tumesoma,
tumechambua maoni ya wengi, wapo waliotaka iwe cheti, wengine diploma, wengine
digrii, wapo waliotaka PhD na wapo waliotaka iwe mtu yeyote nayejua tu kusoma na
kuandika. Serikali imesimama katikati ya maoni hayo. Sifa ya chini kabisa kwa
kuanzia itakuwa ni diploma ya uandishi wa habari” Amesema Nape
Waziri
Nape amesema pia kuwa sheria hiyo imeshaanza kutumika tangu Desemba 31 mwaka
2016, ambapo yeye kama Waziri mwenye dhamana alishatoa tangazo katika gazeti la
serikali.
Aidha
kuhusu wasio na sifa hiyo, Waziri Nape amesema kuwa serikali imetoa kipindi cha
mpito cha miaka mitano ili waandishi wasiokuwa na sifa hiyo, waliopo sasa na
watakaoingia kwenye taaluma hiyo, wakasome ili wawe wamepata sifa hiyo.
Amesema
katika utekelezaji wa sheria hiyo, kuna taasisi ambazo tayari zipo,
zitaongezewa majukumu au kazi zake kuhuishwa, pia kuna vyombo vipya
vitaanzishwa na kuna taratibu mpya za kiutendaji zitaandaliwa.
Kuhusu
manufaa ya sheria hiyo, Nape amesema kuanza kutumika kwa sheria hiyo ni jambo
muhimu kwa tasnia hiyo kwa kuwa ni ruhusa ya kuanza kwa mchakato wa kuifanya
taaluma ya habari kuwa taaluma kamili yenye sifa mahsusi na maadili
yaliyokamilika pamoja na kuwa na vyombo vya kusaidia utekelezaji wake.
Sheria
hiyo ilisainiwa na Rais Magufuli Novemba 16 mwaka 2016, na siku mbili baadaye
ilichapishwa kwenye gazeti la serikali baada ya muswada wake kupitishwa na
Mkutano wa 5 wa bunge mwezi Novemba 2016.
No comments:
Post a Comment