Jumla
ya wanafunzi hewa 65,198 wamegundulika kuwepo katika shule za msingi na
sekondari nchini, ambako idadi ya wanafunzi hao isingebainika kiasi cha Sh
milioni 931.3 zingepelekwa shuleni kuhudumia wanafunzi hewa kwa mwaka wa fedha
2016/2017.
Katika mkutano na waandishi wa
habari jana mjini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene (Pichani Juu) alisema kati ya wanafunzi hao
wa shule za msingi ni 52,783 na sekondari ni 12,415.
Simbachawene alisema kazi ya uhakiki
wa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari ilifanyika mikoa yote nchini
kutokana na agizo la Ofisi ya Rais, Tamisemi kwa makatibu tawala wa mikoa yote
ya Tanzania Bara.
Alisema waliagizwa kuhakiki idadi ya
wanafunzi katika shule zote za msingi na sekondari kwa kulinganisha taarifa
ilivyokuwa Machi mwaka huu wakati wa ujazaji wa madodoso ya takwimu za shule za
awali, takwimu za shule za msingi, sekondari na nyaraka za mahudhurio ya
wanafunzi.
Alieleza kuwa taarifa za idadi ya
wanafunzi kabla ya kuhakiki Machi 2016, zilionesha kulikuwa na wanafunzi
9,746,534 wa shule za msingi na wanafunzi 1,483,872 wa shule za sekondari.
“Baada ya uhakiki tuliofanya
Septemba mwaka huu, inaonesha kuwepo wanafunzi 9,690,038 wa shule za msingi na
wanafunzi 1,429,314 wa shule za sekondari,”
alieleza na kuongeza kuwa uchambuzi umeonesha kuwa wanafunzi 52,783 wa shule za
msingi na wanafunzi 12,415 wa sekondari hawakutolewa maelezo ya uwepo wao
shuleni.
Alisema kwa tafsiri rahisi hao ni
wanafunzi hewa kwa shule za msingi na sekondari nchini, ambao idadi hiyo ya
wanafunzi hewa kama isingebainika kwenye uhakiki huo na kupelekwa fedha, Sh
milioni 931.3 zingepelekwa shuleni kuhudumia wanafunzi hewa katika mwaka wa
fedha 2016/2017.
Alisema kati ya fedha hizo Sh
milioni 527.8 ni kwa shule za msingi na Sh milioni 403.4 ni kwa shule za
sekondari.
Aliitaja mikoa inayoongoza kuwa na
wanafunzi hewa ni Tabora (12,112), Ruvuma (7,743), Mwanza (7,349), Dar es
Salaam (4,096), Kagera (4,763), Rukwa (4,054), Singida (3,239), Kilimanjaro
(2,594), Kigoma (2,323), Njombe (2,307), Simiyu (2,081) na Arusha (1,923).
Mikoa mingine ni Mara (1,855), Tanga
(1,378), Geita (1,281), Morogoro (1,172), Mtwara (882), Mbeya (786), Shinyanga
(695), Songwe (512), Manyara (330), Dodoma (284), Lindi (281), Pwani (187),
Iringa (161) na Katavi (0).
Waziri huyo alisema wanafunzi hewa
walianza wakati serikali ilipoanza kupeleka fedha shuleni kama ruzuku.
Alisema Sh bilioni 27 zimekuwa
zikipelekwa kila mwezi kama ruzuku ya uendeshaji shule za msingi na sekondari
na posho ya madaraka kwa ajili ya wakuu wa shule na walimu wakuu, lakini baadhi
ya walimu waliamua kuongeza idadi ya wanafunzi ili wapate fedha zaidi.
“Huu ujinga unaweza kufanywa hata
katika ngazi ya wizara ni jambo la uchunguzi, zile fedha hazipiti Tamisemi
zinakwenda moja kwa moja shuleni,” alieleza
na kuongeza kuwa hatua za kinidhamu zinaendelea kuchukuliwa kwa wale wote
waliosababisha uwepo wa wanafunzi hewa na Tamisemi inaendelea kuhakiki takwimu
zilizowasilishwa.
“Serikali haitegemei tena kuwepo
suala la wanafunzi hewa. Naagiza makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa
mamlaka za serikali za mitaa na wakuu wa shule kuhakikisha suala la wanafunzi
hewa halijitokezi tena katika shule zote za msingi na sekondari,” alibainisha Simbachawene.
No comments:
Post a Comment