Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango amewatoa
wasiwasi watanzania juu ya kodi ya ushuru wa bidhaa katika miamala ya benki na
simu za mkononi kwamba haitawaathiri wao ila makampuni ya simu.
Mhe. Mpango ameyasema hayo Jana
mjini Dodoma alipokuwa akitolea ufafanuzi taarifa za upotoshaji zinazoenezwa
kwenye mitandao ya kijamii kuhusu namna Serikali itakavyotekeleza Bajeti ya
mwaka 2016/2017 iliyopitiswa jana na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kwa sasa sheria
inatamka kwamba ada itatozwa katika kutuma fedha tu, hata hivyo baadhi ya
kampuni za simu na benki zimekuwa zikitumia mwanya wa sheria hiyo kupunguza
wigo wa kodi kwa kutoza ada wakati wa kupokea,” alisisitiza Mhe.
Mpango.
Mhe. Mpango aliendelea kufafanua
kuwa, kwa kuwa makampuni ya simu na benki yamekuwa yakitoza ada wakati wa
kupokea fedha huku serikali haiwatozi kodi kwa fedha zinazopokewa, hivyo basi
Serikali imeamua kutoza ushuru kwenye ada ya kutuma na kupokea fedha au vyote
kwa kadri itakavyotozwa.
Aidha Mhe. Mpango alisisitiza kwa
kusema kuwa ushuru huo utalipwa na benki na kampuni ya simu na siyo mtumiaji au
mpokeaji wa fedha katika miamala itakayofanyika.
Hivyo basi Waziri Mpango ameitaka
Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuhakikisha kwamba tozo
hiyo inaendana na uhalisia wa huduma inayotolewa kwa kufanya ukaguzi wa miamala
ya makampuni ya simu kabla na baada ya tozo ili yasihamishie mzigo kwa
mtumiaji wa mwisho.
Kuhusu suala la kulipa kodi Mhe.
Mpango amewasisitiza wananchi kulipa kodi kama inavyotakiwa ili Taifa liweze
kujenga uwezo wa kujitegemea na kuwaletea wananchi wake maendeleo ya kweli kwa
kuwa hiyo ndio dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano.
No comments:
Post a Comment