Mahakama Kuu
Kanda ya Iringa, jana iliahirisha kesi ya mauaji ya mwanahabari, Daud Mwangosi
inayomkabili askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Iringa (FFU),
Pasificus Simon hadi leo.
Kesi hiyo iliahirishwa baada ya upande wa Serikali kufunga
ushahidi wake. Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa Februari 12, mwaka 2012, leo
inaendelea kwa upande wa utetezi kuleta mashahidi wake mbele ya Jaji Paul
Kihwelo anayeisikiliza.
Katika kesi hiyo ambayo haikuchukua muda mrefu mahakamani
hapo jana, mawakili wa Serikali wakiongozwa na Sandy Hyra na Ladislaus Komanya
walisema wamefunga ushahidi kwa mashahidi wanne wa awali.
Baada ya wakili wa utetezi, Rwezaura Kaijage kukubaliana na
maombi ya upande wa Serikali kufunga ushahidi wao, Jaji Kihwelo aliiahirisha
kesi hiyo hadi leo.
Awali, mtuhumiwa Simon alifikishwa mahakamani hapo akiwa
chini ya ulinzi mkali wa polisi ambao hawaruhusi apigwe picha na waandishi wa
habari.
Mwangosi aliuawa kwa kupigwa bomu Septemba 2, 2012 katika
Kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi alipokuwa akiwajibika kwa kazi za kihabari
wakati wa ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
No comments:
Post a Comment