KAMPUNI
ya Wengert Windrose Safaris (Tanzania) Limited (WWS), imesema kauli iliyotolewa
na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe (Pichani kushoto)kwamba Mahakama Kuu
ilitoa amri kwa waziri ikimtaka kuirudishia Green Miles Safari Co. Limited
(GML) kibali cha uwindaji na kitalu ambacho kinaendeshwa na WWS sio za kweli.
Taarifa
ya WWS iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari ilifafanua kuwa hakuna uamuzi
wowote uliotolewa na Mahakama ukitamka au kuamua kwamba GML ndio mmiliki halali
wa kitalu cha uwindaji ambacho sasa kinaendeshwa na WWS.
Waziri
Maghembe alitoa kauli hiyo wiki iliyopita wakati anajibu hoja za wabunge
bungeni. Kampuni hiyo pia ilisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari
kuwa Mahakama haikuwahi kuamuru Wizara ya Maliasili na Utalii kuirudishia GML
leseni ya uwindaji na vitalu vya uwindaji vilivyonyang’anywa kutokana na
maofisa wake kudaiwa kushiriki uwindaji haramu katika pori la uwindaji la
Selous.
Taarifa
hiyo ilifafanua kwamba ukweli kuhusu jambo hilo ni kwamba Agosti 28, WWS ndio
ilifungua shauri la madai Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara dhidi ya Wizara ya
Maliasili na Utalii, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na GML.
Ilieleza
kuwa katika shauri hilo WWS ilikuwa ikipinga uamuzi wa waziri kubadilisha jina
la kitalu kinachoendeshwa na WWS ili kutoa mwanya wa kitalu hicho kupewa GML.
“Walalamikiwa wote hao hawakuwasilisha utetezi wao mahakamani.
WWS
imeshtushwa na kauli ya Waziri wa Maliasili na Utalii kwamba Mahakama Kuu
Kitengo cha Biashara ilitoa amri kwa waziri ikimtaka kuirudishia GML kibali cha
uwindaji na vitalu vya uwindaji. Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara haijawahi
kutoa uamuzi kama huo.
“Vilevile
tumesikitishwa na kauli ya Waziri kwamba WWS ilikataa kuhama katika kitalu
hicho kwa madai kwamba kitalu hicho ndicho kilikuwa bora zaidi na kwamba
ilikuwa imewekeza zaidi katika kitalu hicho, hivyo isingekuwa tayari kuhama
hata kama Serikali haikuipa kitalu hicho.“Tunasema kwamba kauli hiyo si ya
kweli. Kampuni ya WWS haijawahi kutoa kauli kama hiyo mahali popote au kwa mtu
yeyote. Tunasema kwamba WWS iliiomba wizara kitalu hiki kwa kipindi cha mwaka
2013 - 2018 na wizara ikaipa kampuni yetu kitalu hiki,” ilisema taarifa hiyo.
WWS
ilifafanua kuwa ililazimika kufungua shauri la madai Na. 113 la mwaka 2013
katika Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara kupinga kitendo cha Waziri kutaka
kuwanyang’anya kitalu hicho baada ya kuwa wameshapewa kwa kisingizio cha
kubadilisha jina la kitalu.
“Shabaha
ya kubadilisha jina la kitalu ilikuwa imelenga kuipokonya kampuni yetu kitalu
hiki baada ya kuwa tumemilikishwa kihalali na Serikali,” ilisema sehemu ya
taarifa hiyo. Taarifa ilifafanua kuwa tangu kupewa kitalu hicho mwaka 2013,
Serikali imewawekea notisi za kulipa ada za vitalu kwa jina la Lake Natron
Controlled Area kama ilivyokuwa siku zote, na wameendelea kulipia ada za kitalu
hicho kwa Serikali kwa kutumia jina hilo hilo tangu mwaka 2013 hadi leo hii.
Taarifa
iliongeza kuwa serikali imewapa vibali vya kuendesha shughuli zao kama kupeleka
wageni na wafanyakazi wao kuingia humo kwa kutumia jina hilo.
No comments:
Post a Comment