Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kuanza ziara ya kuishtaki
Serikali kwa wananchi kuhusiana na utumbuaji majipu usiofuata maadili ya kazi
na kutoonyeshwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya televisheni ya vikao vya
Bunge.
Mratibu wa ziara hiyo, Singo Benson
alisema ziara itaanza Juni 7 katika Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga na
kuendelea mikoa mingine, lengo ni kuelimisha wananchi juu ya ubakwaji wa
demokrasia.
“Wananchi wananyimwa haki ya msingi
ya kutoona matangazo ya Bunge moja kwa moja na hakuna sababu ya msingi iliyotolewa,
hivyo lazima tuwaelimishe na tuwatetee wananchi haki zao,” alisema Benson.
Aliongeza kuwa katika utumbuaji
majipu unaofanyika, umekuwa kwa asilimia kubwa ukilenga majipu madogo (viongozi
wa chini) na kuacha viongozi wakubwa mafisadi bila kuchukuliwa hatua yoyote.
Benson alitoa mfano wa ubakwaji wa
demokrasia akisema ni kitendo cha Serikali kuingilia mihimili mingine, Bunge na
Mahakama, ambapo kwa Bunge Serikali ina daiwa kuingilia uchaguzi wa mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali(PAC) ambaye anatakiwa kutoka
kambi ya upinzani.
Alisema ziara hiyo itakayojumuisha
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent
Mashinji itakuwa na awamu nne nchi nzima huku wabunge wote na wajumbe wakuu wa
chama watashiriki, akiwamo aliyekuwa mgombea urais 2015, Edward Lowassa.
Awamu ya kwanza itakayochukua siku
14 itaendelea kwa kugawana maeneo na kundi moja la viongozi wa Chadema litaenda
maeneo ya Chato, Katoro, Busanda, Biharamulo, Muleba, Bukoba Mjini, Karagwe,
Ngara na Geita; Kundi la pili Shinyanga mjini, Meatu, Maswa, Bariadi, Lamadi,
Musoma Mjini, Bunda, Tarime na kuhitimisha Mwanza Mjini.
Benson ambaye pia ni Mkurugenzi wa
Uratibu na Mafunzo wa Chadema, alieleza kuwa awamu ya pili itahusisha nyanda za
juu kusini na kati, awamu ya tatu itakuwa mikoa ya kaskazini na kusini na
kuhitimisha jijini Dar es Salaam.
“Ziara hizi zinawakaribishwa wabunge
na wanasiasa wa vyama vyote wenye lengo la kutetea haki za wananchi kwa
viongozi waliowachagua,” alieleza
Benson.
No comments:
Post a Comment