YANGA SC imefanikiwa kwenda hatua ya
makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika licha ya kufungwa bao 1-0 na
wenyeji Sagrada Esperanca jioni ya jana katika Uwanja wa Esperanca mjini Dundo, Angola.
Kwa matokeo, hayo Yanga inakwenda hatua ya
makundi kwa ushindi wa jumla wa 2-1, baada ya awali kushinda 2-0 Dar es Salaam,
mabao ya Simon Msuva na Matheo Anthony.
Matokeo hayo si tu yanamaanisha Yanga inatinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza katika historia yake, bali pia inakuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufika hatua hiyo ya michuano hivyo.Awali ya hapo, Yanga imewahi kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998, ikafuatiwa na mahasimu, Simba SC mwaka 2003.
Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na marefa wa Madagascar, Hamada el Moussa Nampiandraza, aliyesaidiwa na Velomanana Ferdinand Jinoro na Jean Thierry Djaonirina, hadi mapumziko, tayari wenyeji walikuwa wamekwishajipatia bao lao hilo.
Bao hilo lilifungwa na mkongwe Arsenio Sebastiao Cabungula maarufu kama ‘Love Kabungula’ dakika ya 25, baada ya mabeki wa Yanga kufanya uzembe kidogo.
Yanga walitulia baada ya bao hilo, licha ya marefa kuonekana kabisa kupendelea wenyeji na wakafanikiwa kumaliza dakika 45 za kwanza wakiwa nyuma kwa bao hilo moja tu.
Kipindi cha pili, Yanga waliachana na mchezo wa kujihamia na kufunguka kuanza kushambulia, hali ambayo ilipunguza kasi ya wapinzani wao.Kocha Mholanzi alimtoa kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko baada ya kuumia na kumuingiza Deus Kaseke dakika ya 69.Mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma alipoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 72.Kipa Deo Munishi 'Dida' akaokoa penalti iliyotolewa baada ya Nahodha, Cannavaro kumuangusha mchezaji wa Sagrada Esperanca. Hata hivyo Nahodha Canavaro alitolewa kwa kadi nyekundu dk ya 92 kwa tuhuma za kucheza vibaya.
Refa aliongeza dakika tano baada ya kutimia dakika 90 na Nahodha Cannavaro akatolewa kwa kadi nyekundu pia dakika ya 90 na ushei.Vurugu zikaibuka dakika ya mwisho ya dakika za nyongeza na kipa wa Yanga, Dida akapigwa jiwe na mchezo kusimama kwa muda. Askari Polisi waliingia uwanjani kutuliza fujo na mchezo ukaendelea kwa sekunde kadhaa kabla ya refa kumaliza.
Ikumbukwe, Yanga iliangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.Yanga ilianza vizuri tu kwa kuzitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla ya kuitoa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
KIKOSI CHA YANGA KILIKUWA;
1. Deo Munishi ‘Dida’,
2. Juma Abdul,
3. Oscar Joshua,
4. Vincent Bossou,
5. Nadir Haroub ‘Cannavaro’,
6. Mbuyu Twite,
7. Simon Msuva/Geoffrey Mwashiuya dk90+4,
8. Thabani Kamusoko/Deus Kaseke dk69,
9. Donald Ngoma,
10.Amissi Tambwe/Kevin Yondan dk90
11.Haruna Niyonzima.
++++++++++++++++++++++++++++
TIMU ZILIZOTINGA
HATUA YA MAKUNDI:
-Yanga
-TP Mazembe - Congo DR
-MO Bejaia – Algeria
-ES sahel – Tunisia
-Medeama – Ghana
**Bado 3
**Droo ya Kupanga Makundi Mawili ya
Timu 4 kila moja kufanyika Tarehe 24 Mei huko Cairo, Egypt
**Mechi za Makundi kuanza Juni 11
++++++++++++++++++++++++++++
No comments:
Post a Comment