Ikiwa ni siku tatu tangu Mkurugenzi wa Habari Uenezi na Mawasiliano ya
Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Hamad Masoud Hamad (PICHANI), atangaze kuwa baadhi ya
wananchi wa Zanzibar wanakimbilia porini kuhofia usalama wao, ametiwa mbaroni.
Kukamatwa kwa Masoud
sasa kunafanya idadi ya viongozi wa chama hicho waliotiwa mbaroni na kuhojiwa
polisi kufikia wanne tangu kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 28,
mwaka jana.
Viongozi wengine
waliohojiwa na Polisi na kuachiwa kwa dhamana ni Naibu Katibu Mkuu, Nassor
Ahmed Mazrui, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Omar Alin Shehe na mshauri wa
mikakati wa chama hicho, Eddy Riyami.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi
Unguja, Mkadam Khamis Mkadam, jana alithibitisha kukamatwa kwa Masoud, ambaye
ni Waziri wa zamani wa Miundombinu na Mawasiliano katika Serikali ya Umoja wa
Kitaifa.
Alisema kiongozi huyo
alikamatwa na kitengo cha upelelezi nyumbani kwake mtaa wa Mbweni mjini
Zanzibar jana.Alisema kwa sasa anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Mwembe
Madema ili kusadia uchunguzi juu ya taarifa alizotoa katika mkutano wake na
waandishi wa habari na kuzungumzia hali ya amani ya Zanzibar na wananchi wake.
“Tunamshikilia kwa uchunguzi, kuna mambo ya
msingi tunaona yanahitaji kufanyiwa uchunguzi na yeye kusadia polisi uchunguzi
wake,” alisema Mkadam.
Kufuatia kukamatwa huko
kwa Masoud, CUF imelaani kitendo hicho na kusema kuwa kamata kamata hiyo
inawalenga viongozi wa chama hicho na wanachama wake pekee.
Naibu Katibu Mkuu wa
chama hicho, Mazrui alisema matukio yote ya uvunjifu wa amani yaliyotokea
visiwani hapa, yamekuwa yakihusishwa na CUF na Jeshi la Polisi huwakamata
viongozi wa chama hicho pekee.
“Tunasema huu ni uonevu wa hali ya juu,
maana viongozi na wafuasi wa CUF pekee ndio wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi,
hii yote inatokana na uchaguzi wa marudio, hivyo kutoshiriki kwetu kwa
uchaguzi isiwe sababu ya kuadhibiwa,” alisema.
Aidha, alisema suala la
kushiriki au kutoshiriki katika uchaguzi ni hiari ya mtu, hivyo kwa wale ambao
hawatashiriki uchaguzi huo, wasiadhibiwe wala wasidhalilishwe na wale ambao
wametangaza kushiriki waende wakapige kura.
Kwa upande wa mke wa
Masoud, Rahma Issa, alisema askari kazu wasiopungua sita wakiwa na silaha za
moto mbili walifika nyumbani jana saa moja asubuhi na kudai wanamhitaji mumewe.
Alisema baada ya
kubisha hodi, kijana wake mmoja alifungua mlango na kisha askari watatu
waliingia ndani mmoja akiwa na silaha ya moto kifuani.
“Baada ya kuamshwa na kutoka chumbani
walimwambia yupo chini ya ulinzi anahitajika kituo cha polisi,” alisema Rahma.
Hata hivyo, alisema
baada ya kumkamata, hawakumwambia sababu ya kukamatwa kwake, lakini baada ya
kuwauliza wanampekeka kituo gani walimwabia Kituo cha Polisi Mwembe Madema,
Zanzibar.
Naye Mkurugenzi wa
Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe, alisema vitendo vya kukamatwa
viongozi wa CUF ni mwendeleo wa Serikali ya CCM kuwanyanyasa viongozi na
wanachama wake chama hivyo visiwani hapa.Alisema vitendo vinavyoendelea
kufanywa na Jeshi la Polisi vinakwenda kinyume cha misingi ya demokrasia na
haki za binadamu.
Shehe alisema matunda
ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya kujenga amani na umoja wa kitaifa yameanza
kuvurugwa tangu kuingia mgogoro wa uchaguzi mkuu.
No comments:
Post a Comment