Serikali ya Uingereza kupitia shirika lake la kuchunguza
makosa ya jinai (AFO), imeibua kashfa ya rushwa katika ununuzi wa dhamana (hati
fungani) ya serikali katika kipindi cha uongozi wa aliyekuwa Rais Jakaya
Kikwete.
Madai hayo yametolewa jijini Dar es
Salaam jana na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe (Pichani), katika
taarifa yake aliyoisambaza kwenye vyombo vya habari jana.
Katika taarifa yake hiyo, Zitto
alidai kuwa biashara hiyo iliyofanyika kati mwaka 2011 na 2012, iliyohusisha
serikali na benki ya Standard Group ya Afrika Kusini kupitia Stanbic ya
Tanzania ilikuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 600 (sawa Sh. Tanzania
trioni 1.2).
Benki ya Standard Group ambayo ni
benki mama ya Stanbic Tanzania, imekiri makosa hayo na kukubali kulipa faini ya
Dola milioni 25.2 (sawa na Sh. bilioni 54 ) kwa kosa hilo.
Ilikubali kulipa faini hiyo mbele ya
Jaji Lord Justice Leveson, wakati shauri hilo liliposikilizwa jana kwenye
Mahakama ya Southwark nchini Uingereza.
Benki hiyo ilikubali shauri hilo
limalizwe kwa njia ya muafaka baada ya kukiri ilitoa kiasi cha fedha ili
kuwahonga maofisa wa Tanzania kinyume na Sheria ya Rushwa ya Uingereza ya mwaka
2010 kufanikisha mpango wao.
Pia benki hiyo imekubali kulipa
kiasi cha Dola milioni saba (sawa na Sh. bilioni 15.1) kwa Serikali ya Tanzania
kama fidia ya shauri hilo baada ya kubainika walihonga baadhi ya maofisa wa
Tanzania kufanikisha mpango huo.
Hata hivyo, fedha hizo
hazitakabidhiwa moja kwa moja kwa Serikali ya Tanzania bali zitapitishwa kwenye
Wizara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza ili kupangiwa kazi ya kufanya.
Pia benki hiyo inatakiwa kulipa
kiasi cha pauni 300,000(sawa na Sh. milioni 974) ikiwa ni gharama za shauri
hilo kusikilizwa nje ya mahakama.
Katika taarifa yake, Zitto alitaka
mamlaka zenye kuchunguza sakata hilo ikiwamo Benki Kuu ya Tanzania, Kitengo cha
Kudhibiti Biashara Haramu ya Fedha (FIU) Tanzania na Taasisi ya Kupambana na
Kuzuia Rushwa nchini (Takukuru) waungane na SFO kutoa taarifa za chunguzi
huo na sababu ya kutoziweka hadharani mapema.
Aliomba vyombo vya sheria
kuwachukulia hatua wote waliohusika na upotevu fedha hizo za Watanzania.
Alisema hati fungani hiyo ya
serikali iliuzwa na serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa benki hiyo ya kigeni
ambayo ni miongoni mwa kundi la mabenki ya Afrika ya Kusini, yenye makao makuu
yake London, Uingereza.
Alisema ni jambo la kawaida duniani
serikali kuuza dhamana zake za hati fungani, lakini kwa Tanzania uligubikwa na
harufu ya rushwa na kuisababishia nchi hasara.
Alidai kuwa kwa mujibu wa uchunguzi
huo, sehemu ya fedha hizo hazikuingia kwenye akaunti za Serikali ya Tanzania na
pia gharama za hati fungani hiyo zilipaishwa kupitia wakala wa kati.
Kutokana na upaishaji wa gharama
hizo, takriban Dola milioni 60 zilitolewa kwa maofisa waliothibitisha biashara
hiyo.
Zitto alimuomba Rais Dk. John Magufuli,
kuingilia kati suala hilo akisema jambo hilo lina maslahi mapana ya nchi, hasa
ikizingatiwa na uzoefu katika masakata kama hayo yanayohusisha nchi za kigeni,
kama ununuzi wa rada, vyombo vya uchunguzi vya hapa nchini, vilitoa majibu ya
kutokuwapo kwa rushwa na kisha kuja kuthibitishwa na Serikali ya Uingereza.
“Baada ya kuthibitishwa na
Uingereza, serikali yetu ilirudishiwa sehemu ya fedha zilizozidi kwenye
manunuzi ya rada, ni vyema Rais Magufuli akaliingilia kati,” alisema Zitto.
Alisema ACT-Wazalendo inasubiri
taarifa ya makubaliano kati ya SFO na benki mama ya iliyonunua hati fungani
hiyo ili ashauri zaidi hatua za kuchukua.
“Ikumbukwe kuwa Benki ya…(anaitaja
jina), ilihusika na kashfa ya Tegeta Escrow na mpaka sasa haijachukuliwa hatua
zozote kama ilivyoagizwa na Bunge. Benki hiyo imewaficha waliochota fedha za
Escrow mpaka leo,” alisema Zitto.
Alisema kashfa hiyo iliwafanya
washauri uongozi wa benki hiyo hapa nchini kuondolewa na kurejeshwa nchini
Uingereza kwa hatua zaidi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Hazina,
Ramadhani Kijja, alilieleza Nipashe kuwa halifahamu suala hilo na kwamba kwa
sasa hana maelezo yoyote juu ya jambo hilo.
“Kama Zitto ndiye katoa hiyo
taarifa, mimi sina na wala siwezi kuizungumzia kwa sasa,” alisema Kijja.
Mkurugenzi wa Takukuru Dk. Edward
Hoseha, alipopigiwa simu yake ya mkononi kuulizwa suala hilo, hakuwa tayari
kulizungumzia akisema ni jambo linalohitaji ufafanuzi wa kutosha.
“Ukitaka ufafanuzi, njoo tuonane,
ofisi yangu ipo wazi, it is difficult to talk (ni vigumu kuzungumza) kuhusu
jambo hilo kwa simu, hautanitendea haki, njoo tutaelezana vizuri tu,” alisema
Dk. Hoseah.
Alipotafutwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, George Masaju, kuzungumzia suala hilo, hakupatikana baada ya simu
yake kuita bila kupokelewa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment