Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli (Pichani) amewatakia heri watanzania wote katika siku ya UKIMWI duniani inayofanyika
leo tarehe 01 Desemba, 2015
Katika salamu hizo Rais Magufuli amesema jukumu la kupambana
na UKIMWI linamhusu kila mtu na hivyo amewasihi watanzania kuzingatia mahubiri
ya viongozi wa dini, na pia kuzingatia elimu itolewayo na wataalamu wa afya
katika kujikinga na ugonjwa huo.
Dkt. Magufuli amewahakikishia waathirika wa ugonjwa wa
UKIMWI kuwa Serikali itaendelea kuimarisha tiba na huduma zao na ndio maana
alielekeza fedha zote zilizopatikana kwa kufuta shamrashamra za maadhimisho
hayo zielekezwe kununulia dawa za kurefusha maisha kwa wagonjwa wa UKIMWI.
Rais Magufuli ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa elimu
kwa umma juu ya kuepukana na maambukizi mapya na kuhimiza watu kujitokeza kwa
hiari kupima afya zao.
Amewaomba viongozi katika ngazi zote kuendelea kuwahimiza
akinamama wajawazito kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kuchunguza
afya zao ili wale ambao watakaogundulika kuathirika na ugonjwa huo, wapatiwe
dawa za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Aidha, Rais amewapongeza wadau wa ndani na nje ya nchi wanaoshirikiana
na Serikali katika kupambana na janga la UKIMWI na kuwaomba wadau hawa wa
maendeleo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali.
Imetolewa na
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano,
IKULU
30 Novemba, 2015

No comments:
Post a Comment