SERIKALI imesema siku ya
Desemba 9 iliyopangwa kuwa siku ya usafi wa mazingingira haitawafanya
wafanyakazi wa utumishi wa umma kwenda kazini bali wataungana na wananchi
kwenye maeneo wanayoishi kwa kufanya usafi wa mazingira.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa
Idara ya Habari Bw Assah Mwambene (Pichani) alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
leo jijin Dar es salaam na kusema kwamba Watumishi wa Umma wanatakiwa
wabaki nyumbani na kufanya usafi katika maeneo yao na yale watakayo
pangiwa na viongozi wa mitaa wanayoishi.
“Kila mwananchi ahakikishe eneo lake
ni safi”Alisema Mwambene.
Mkurugenzi amesema kuwa Watumishi wa
Umma hawataenda kazini badala yake watabaki nyumbani na kufanya
usafi kwa kushirikiana na wananchi kusafisha maeneo yanayozunguka mitaa
wanayoishi ikiwemo hospitali,kuzibua mitaro iliyoziba pamoja na kuzoa taka
zilizolundikana sehemu ambazo sio rasmi.
Ameongeza kuwa muongozo kuhusu namna
zoezi la usafi litakavyotekelezwa umeshatolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu
TAMISEMI kwa Uongozi wa Mikoa hadi Mitaa na kilichobaki ni utekelezaji tuu
wa agizo hilo kwa kila mwananchi sehemu anayoishi,anayofanyia shughuli nyingine
za kila siku kuhakikisha anafanya usafi.
Aidha Mkurugenzi amewataka viongozi
wa kila eneo kutengeneza utaratibu mzuri ambao utafanikisha zoezi la
usafi kufanikiwa kwa kuhakikisha wanasimamia kwa ukamilifu na kuwahimiza
wananchi kuwa na tabia ya kusafisha maeneo wanaoishi kwa kuwa ni wajibu wao
kufanya hivyo.
Hata hivyo tarehe tisa disemba kila
mwaka huwa ni siku ya kusherehekea Uhuru wa Tanganyika uliopatikana miaka hamsini
na nne iliyopita lakini kwa mwaka huu itaadhimishwa kwa kufanya usafi nchi
nzima.

No comments:
Post a Comment