AWALI
ya yote niwape hongera wana Simba wote kwa uvumilivu mkubwa mlionao, hasa
katika kipindi hiki kigumu ambacho mnapitia.
Kipindi kigumu kwa maana mbili
kubwa. Kwanza najua wengi hamridhiki na nafasi tuliyopo hivi sasa kwenye
msimamo wa ligi kuu inayoendelea nchini na pia wengi mmekuwa na sintofahamu
kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea nje ya uwanja, hususan suala la
kuvamiwa kwa eneo linalotarajiwa kujengwa uwanja linalomilikiwa na Klabu ya
Simba kule Bunju jijini Dar es Salaam.
Naomba nianze na suala la wapenzi
kutoridhika na maendeleo ya timu uwanjani, hususan kuwa kwenye nafasi ya nne
kwenye msimamo wa ligi kuu.
Siyo siri, Simba inapita katika
kipindi kigumu sana, lakini kiukweli nafasi tuliyopo kimsimamo, siyo mbaya hata
kidogo, ukilinganisha na klabu zilizopo juu yetu.Tofauti yetu na timu
inayoongoza Ligi Kuu Tanzania Bara ni pointi nne tu huku kila timu ikiwa
imecheza michezo tisa.
Wapo wanaosema timu haichezi soka
linaloburudisha, pia wapo wanaokwenda mbali zaid kwa kusema kwenye safu ya
ushambuliaji kuna udhaifu mkubwa.
Kwa jicho langu, kuna eneo
nakubaliana na baadhi ya mitazamo ya wakosoaji, ila niwaambie uongozi unazijua
changamoto zote hizo, hususan kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ambayo hata
Kocha wa Simba, Dylan Kerr alitaka hivyo.
Taarifa njema kwa wana Simba ni
kurejea kwa mchezaji wake Mkenya, Paul Kiongera, aliyekuwa kwa mkopo kwenye
timu ya KCB ya nchini Kenya.Lakini pia usajili wa Brian Majwega, mchezaji wa
kimataifa wa Uganda aliyekuwa Azam FC, naye ataanza rasmi kuitumikia Simba mara
ligi itakapoanza kwenye raundi ya kumi baadaye mwezi huu.
Mimi naamini kwa usajili huu, Simba
itakuwa imepata suluhisho kwenye safu yake ya ushambuliaji, ukizingatia
kupatikana kwa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ya mshambuliaji wetu, Danny
Lyanga, sambamba na usajili wa beki mpya kutoka timu moja inayocheza ligi kuu
nchini.
Naamini kwa usajili huo,
ukichanganya na majembe yetu tuliyonayo, tutafanya vizuri msimu huu.Tunachoahidi
ni kuwapa matarajio yenu, tena kwa nguvu zote, la kuomba ni uhai tu.
La pili, nililopanga kuwaambia
kwenye barua hii fupi, ni suala la uwanja wetu uliopo Bunju.Zimeibuka porojo
nyingi kuhusu uwanja wetu wa Bunju kuvamiwa na baadhi ya watu ambao wamejenga
nyumba kwenye eneo hilo.
Binafsi nilipoziona hizi taarifa
kwenye baadhi ya vyombo vya habari, nilishtuka sana, hata Rais wa Simba, Evans
Aveva, naye alishtuka kupita kiasi na kuamua kuondoka mwenyewe kwenda kujionea
kinachoendelea huko.
Kimsingi hakuna mtu au kikundi
chochote ambacho kimevamia eneo hilo. Kilichoonekana kwa baadhi ya waandishi
waliokwenda eneo hilo ni kuzionyesha nyumba zilizopo pembeni ya eneo la Simba
na kusema kuwa zimejengwa ndani ya eneo letu, lakini siyo kweli.
Wakati mwingine najiuliza unawezaje
kujua mipaka sahihi kama siyo kuwauliza wamiliki halali wa eneo husika au watu
wa manispaa na wale wa ardhi?
Ni kuikosea heshima klabu kwa
kiwango cha juu kuandika habari bila kufanya utafiti na kuwaweka wapenzi wetu
roho juu bila sababu yoyote ya msingi.
Ninalowaomba wanachama na wapenzi
wetu, wapuuze hizo taarifa, ni uongo mkubwa.
Matarajio yetu ni kuona habari za
upotoshaji wa aina hiyo hazijirudii tena na sisi tutaendelea kutoa ushirikiano
kwa vyombo vyote vya habari kwa kuzingatia misingi ya uandishi na utamaduni wa
klabu.
Mwisho…
Ofisa Habari
Simba Sport Club
Haji Manara(Pichani)


No comments:
Post a Comment