
Mtanzania anayedaiwa kuhusika katika shambulizi la
kigaidi lililoua watu 148 katika Chuo Kikuu cha Garissa – Kenya, Rashid Charles
Mberesero, jana alifikishwa mahakamani na kuwekwa kizuizini kwa mwezi mmoja
wakati polisi wakiendelea kukusanya ushahidi dhidi yake.
Mtuhumiwa
huyo ambaye pia anafahamika kwa jina la Rehani Dida alirejeshwa Nairobi kutoka
Garissa alikopelekwa awali kwa ajili ya kuhojiwa baada ya kukiri kujihusisha na
kundi la Al- Shabaab.
Mahakama
jijini Nairobi ilisema jana kuwa mtuhumiwa huyo ambaye hakutakiwa kujibu tuhuma
hizo na wenzake wanne watalazimika kuwa chini ya uchunguzi mkali wa polisi kwa
kipindi cha mwezi mmoja na baadaye wanaweza kusomewa mashtaka ya kuhusika
katika shambulizi hilo lililoua watu hao, wengi wao wakiwa ni wanafunzi.
Haikufahamika
mara moja sababu za kuamuliwa kuwekwa kizuizini kwa muda huo mbali ya taarifa
kueleza kuwa ‘watashikiliwa na polisi tena katika kituo cha siri’.
Mwendesha
Mashtaka, Daniel Karuri aliiambia Mahakama hiyo kuwa Mtanzania huyo ambaye ni
mwanafunzi wa kidato cha tano, alikuwa amepanga safari ya kuelekea Somalia kwa
ajili ya kujiunga na makundi ya kigaidi.
Watuhumiwa
hao ni kati ya 14 waliotiwa mbaroni hivi karibuni baada ya shambulizi hilo la
kigaidi.
Mahakama
hiyo pia imewaamuru washukiwa wengine kuendelea kushikiliwa na polisi kwa muda
wa siku tano hadi 15.
Awali,
Karuri aliiambia Mahakama hiyo kuwa polisi walikuwa wakifuatilia kwa karibu
uhusiano baina ya wale waliofanya shambulizi hilo na mfanyabiashara mmoja
anayemiliki hoteli mjini Garissa. Inasemekana kuwa watu waliotekeleza shambulio
hilo walikuwa wamelala katika hoteli hiyo.
Hakula chakula cha shule
Wanafunzi
wa Shule ya Sekondari ya Kigwe, mkoani Dodoma alipokuwa akisema Mberesero baada
ya kufaulu kutoka Gonja, wamesema hakuwahi kula chakula chochote shuleni kwa
kipindi cha mwezi mmoja aliokaa akisubiri kuhamishwa na kubadilishiwa mchepuo
wa masomo.
Wakizungumza
na mwandishi wetu shuleni hapo jana, wanafunzi wa kidato cha tano, Yoram James
na Thomas Godwin, walisema siku zote alizoishi shuleni hapo alikuwa akila kwa
mama lishe jirani na shule hiyo.
“Lakini
alikuwa na mkarimu kwetu wakati mwingine alikuwa akitununulia maandazi ya
kunywea chai,” alisema Yoram.
Hata
hivyo, walisema kutokana na upole wake, jinsi anavyoongea na kutumia muda mrefu
msikitini, walimpa jina la Ustaadhi.
“Alikuwa
akienda mjini mara kwa mara, nadhani alikuwa akiomba ruhusa kwa walimu au
alikuwa akitoroka,” alisema Thomas.
Thomas
alisema Rashid alikuwa akipenda kucheza mpira wa miguu kwa hiyo alitenga muda
wake kwa ajili hiyo.
Uhamisho wake
Mkuu wa
Shule hiyo, Ramadhan Bakari alisema ofisi ya elimu mkoa ilituma taarifa ya
kuwataka wanafunzi wanaopenda kubadilisha mchepuo kuandika barua ya maombi.
“Rashid
alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi watano walioomba kubadilishiwa mchepuo kutoka
Sanaa kwenda Sayansi, walikubaliwa wanne akiwamo yeye,” alisema Bakari.
Hata
hivyo, mwalimu huyo alisema Rashid alikuwa akihangaika ahamishiwe Shule ya
Sekondari ya Bihawana, tangu aliporipoti Kigwe.
“Hatuwezi
kuzungumza kuhusu tabia zake maana hapa hakuishi siku nyingi, alikuwa kama yuko
njiani,” alisema.
“Aliondoka
hapa shuleni kwenda Bihawana Agosti 19, mwaka jana baada ya taratibu
kukamilika,” alisema.
Uvumi wasambazwa
Hofu
imetanda katika maeneo mbalimbali baada ya kusambazwa ujumbe kwenye simu na
mitandao ya kijamii ukidaiwa kutolewa na Umoja wa Mataifa (UN) kutahadharisha
watumishi wake waepuke kukaa katika makundi makubwa na mikusanyiko katika
majiji ya Dar es Salaam, Mwanza na Arusha leo kuepuka mashambulizi ya kigaidi.
Hata
hivyo, Msemaji wa UN, Usiah Ledama alikanusha umoja huo kuhusika na ujumbe huo
akisema ni feki na hauna ukweli wowote.
Kaimu
Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Diwani Athumani alisema hata kama
ujumbe huo ni feki, bado Jeshi la Polisi linachukua tahadhari kuhakikisha Taifa
linakuwa salama.
“Huo
ujumbe uwe feki au wa kweli, lazima tuchukue tahadhari, Tanzania si kisiwa,
tutakuwa salama kwa asilimia 100, kwa hiyo ulinzi unaimarishwa,” alisema.
Alisema
ni lazima kila mtu awe mlinzi wa mwenzake na ahakikishe kuwa anakuwa mzalendo
kwa kutoa taarifa zozote ambazo anadhani zitalisaidia Jeshi la Polisi katika
ulinzi.

No comments:
Post a Comment