Uchaguzi
Mkuu wa kwanza wa vyama vingi ulifanyika mwaka 1995. Wananchi wa Jimbo la
Kilindi walikuwa na fursa adhimu ya kuchagua viongozi imara ili kulijenga jimbo
hili ambalo ni moja kati ya wilaya zilizo nyuma sana kimaendeleo nchini
Tanzania.
Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi ulifanyika mwaka 1995. Wananchi wa Jimbo la Kilindi walikuwa na fursa adhimu ya kuchagua viongozi imara ili kulijenga jimbo hili ambalo ni moja kati ya wilaya zilizo nyuma sana kimaendeleo nchini Tanzania.
Vyama vya upinzani vikiongozwa na NCCR vilikuwa dhaifu kiasi cha kuleta uhakika kuwa CCM itakosa ushindani wa kweli lakini kama ilivyo kwa ile fomula ya tembo kukanyaga sisimizi, CCM ikamsaka na kumpata mgombea msomi aliyebobea kwa kiwango cha juu sana, Juma Salim Kidunda. Kidunda alikuwa na shahada ya uzamili ya uchumi wa kilimo kutoka Chuo Kikuu cha London, Uingereza na alifanikiwa kuwabwaga wagombea kutoka vyama vingine na kuihakikishia CCM ushindi.
Ilipofika mwaka 2000 CCM ilimpa Kidunda jukumu la kuilinda dhidi ya upinzani dhaifu. Ikumbukwe kuwa Kilindi ni ngome muhimu ya CCM na zaidi ya yote vyama vinavyosaka mabadiliko havijafanya kazi ya kujichimbia hapa. Kidunda aliitumia vema fursa hii ya pili akaongoza kwa kura nyingi na kuchaguliwa kuongoza, na huu ni wakati ambapo alijinoa kitaaluma kwenye Chuo Kikuu cha London akichukua shahada ya uzamivu ya uchumi wa kilimo.
Mwaka 2005 ulikuja na mambo mawili muhimu. Kwanza ni kuondoshwa kwa Kidunda katika kuomba ridhaa na nafasi yake kuchukuliwa na mwanamama Beatrice Matumbo Shellukindo. Shellukindo ni mmoja wa wanasiasa machachari kutoka mkoani Tanga na ni mwanamke anayethubutu kufanya jambo analoona linaendana na fikra zake. Mwanamama huyu ni msomi wa kiwango cha shahada ya uzamili (M.A) ya elimu aliyoipata nchini Bulgaria.
Shellukindo alikutana na upinzani mdogo kutoka kwa mgombea pekee kutoka CUF, Fedah Juma. Baada ya kampeni na kura kupigwa mwanamama huyu aliibuka mshindi na kuongeza idadi ya wabunge waliothubutu kusimama majukwaani kupambana na wanaume na kuwashinda. Shellukindo alipata kura 41,505 (asilimia 87.2) na Juma wa CUF akipata kura 6,107 (asilimia 12.8). Kabla ya kuingia kwenye uchaguzi na kushinda nafasi hii adhimu, Shellukindo alikuwa ni mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), nafasi aliyoitumikia mwaka 2004.
Mwaka 2010 ulifika ukiikuta Kilindi chini ya upinzani dhaifu zaidi. Hii ni kwa sababu CUF ambayo ilijengwa na kina Fedah Juma miaka ya nyuma ilikuwa imeporomoka na kuacha ombwe kwa siasa za jimbo hili. Hata hivyo ni Chadema ndiyo ilijikongoja kwa kutumia mtandao uliobakia wa CUF na kujenga nguvu ya umma. Chadema ilimpata Pius Mseja Mbetta bila kujali kuwa angeweza kusimama na Shellukindo wa CCM. Kura zilipopigwa Shellukindo aliongeza ushindi wa CCM kwa asilimia 5 akipata kura 31,077 (asilimia 92.47) na Chadema ikiambulia asilimia 5.37 na kumpa Shellukindo nafasi ya kuwatafutia wananchi wa Kilindi fursa zaidi kama mwakilishi wao.
Inaonekana Shellukindo anajua namna ya kuendesha siasa za Kilindi. Huwezi kuamini kuwa katika Halmashauri ya Kilindi, CCM imepita bila kupingwa katika vijiji vyote 102 na vitongoji vyote vya kata 20 kutokana na vyama vya upinzani kushindwa kusimamisha wagombea. Katika karne hii ni jambo la aibu sana kidemokrasia kukuta eti wilaya nzima upinzani unashindwa kuweka wagombea hata wa mtaa. Viongozi wa vyama vya Ukawa wanapaswa kulichunguza suala hili, inawezekana kabisa kwamba kuna baadhi ya wilaya ambazo viongozi wake wanashirikiana na wakongwe wa CCM kudhoofisha upinzani. Haina ubishi kwamba CCM itapata ushindi mkubwa mwezi Oktoba mwaka huu, kama ni uchaguzi chama hicho kikubwa kimeshaukamilisha mwezi Desemba mwaka jana.
JIMBO LA MKINGA
Jimbo la Mkinga ni sehemu yote ya wilaya ya Mkinga. Jimbo hili lina kata 22, vijiji 105 na vitongoji 768. Kwa upande wa idadi ya wakazi, Mkinga ina watu 118,065 kwa mgawanyo wa wanaume 57,760 na wanawake 60,305 na kila kaya ina wastani wa watu wanne (Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2012).
Mkinga ni moja kati ya maeneo ambayo CCM inayahofia sana mkoani Tanga. Jimbo hili limekuwa na historia imara ya msimamo wa wapiga kura, hapa Mkinga chama chochote kikiweka wawakilishi wasio na ushawishi wananchi hawawachagui kwa hivyo ile michezo ya CCM ya kuweka mtu yeyote ili chama kimsaidie haifanyi kazi.
Mwaka 1995 Mkinga ilijionea siasa zilizokomaa na ushindani ambao uliwavutia wengi. Pamoja na vyama 6 kuweka wagombea lakini ni vyama vitatu ndivyo vilifanya mchuano uwe mgumu, NCCR, CUF na CCM. Pamoja na vyama hivyo kuvutana kiasi hicho usingeliweza kuvikebehi vyama ambavyo havikuwa kwenye mstari wa ushindi yaani UMD, UPDP, NRA na NLD, kwa sababu vyama hivi pia viliweka wagombea thabiti, vyote vinne vilipata asilimia 9 ya kura zote.
Waliokuwa mstari wa ushindi walinyang’anyana kipande kilichobakia ambapo Zahabu Mhilu Dunstan wa NCCR alipata kura 3,176 (asilimia 13.0), Juma Omari Hassani wa CUF akipata kura 4,326 (asilimia 17.7) na Luka Dunstan Kitandula wa CCM aliibuka mshindi wa jumla kwa kura 14,785 (asilimia 60.4) na kuchukua uongozi wa jimbo la Mkinga kwa miaka mitano ya kwanza.
Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 CCM iliandaa mgombea mpya na Dunstan Kitandula akawekwa pembeni. Mbaruk Kassim Mwandoro ndiye alishika usukani kupambana na wapinzani na kufaulu. Alikuwa na kazi ngumu sana ya kupambana na CUF japokuwa mwaka 2000 haukuwa mzuri sana kwa upinzani hapa nchini. Mwandoro akawa mbunge wa pili wa Mkinga na kuipa CCM pumzi za kwenda 2005.
Mwaka 2005 CUF ilikuwa na mtandao uliiongezeka na ilimpata mgombea mzuri, Bakari Kassim Mbega. Mbega ni mmoja wa makada wa CUF waliofanya kazi kubwa ya ujenzi wa chama hicho hapa Mkinga na ana uzoefu wa kutosha katika siasa za Tanga. Vyama vingine havikushiriki katika ngazi ya ubunge na hivyo CCM ilipambana na CUF peke yake, mwakilishi wa CCM akiwa yuleyule Mbaruk Kassim Mwandoro. CUF ilijipatia asilimia 30.0 (kura 11,603) wakati CCM ikiwa na asilimia 70.0 (kura 27,110) ambazo zilimuwezesha Mwandoro kuwa mbunge wa Mkinga kwa mara ya pili.
Kura za maoni ndani ya CCM mwaka 2010 zilimuweka nje Mwandoro. Luka Dunstan Kitandula mbunge wa Mkinga wa mwaka 1995 - 2000 alichukua jukumu na kuweka rekodi ya watu ambao hukaa nje ya uongozi wa ushindani kwa miaka 10 na kisha kurejea tena na kushinda. CCM ilimrejesha Kitandula kwa sababu Mwandoro alikuwa amechokwa na mtu pekee aliyekubalika na kuondoa migawanyiko na makundi ni Kitandula. CUF iliwakilishwa na mkongwe Bakari Kassim Mbega kwa mara nyingine lakini hakufanikiwa kushinda na badala yake akapata asilimia 35.55 (kura 11,252) na kuiacha CCM ikijizolea ushindi wa tabu wa asilimia 62.14 (kura 19,667).
Pia, CUF ilipata madiwani 9 na kuongeza uwakilishi mpana kwa ngazi hiyo lakini kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka jana CUF ilipata vijiji 12 (asilimia 11), Chadema vijiji 2 (asilimia 1.9) na CCM ikibakia na vijiji 91 (asilimia 86.6).
Pamoja na kuwa kinyang’anyiro cha ubunge huwa na upekee wake na kinaweza kutotathminiwa kwa kutumia matokeo ya serikali za mitaa, ni dhahiri kuwa chama kinachochukua vijiji na mitaa kwa asilimia 80 hadi 100 kikipata mgombea mzuri na kusiwe na mgawanyiko kinakuwa na nafasi kubwa kutwaa kiti cha ubunge.
Ndani ya CCM bado mkongwe Luka Dunstan Kitandula ndiye anapewa nafasi huku mshindani wake mkubwa alitarajiwa kuwa Mwantumu Mahiza ambaye
nimeambiwa kuwa anapenda kufanya siasa za “kususa” (wana Mkinga wanajua). Nimejulishwa kuwa kuna wagombea wengi ndani ya CCM wanalitaka jimbo hili jambo linaloweza kugawa kura na kumpa ushindi Kitandula.
Hata hivyo, mwana CCM yeyote atakayepitishwa atakuja kupambana na Bakari Kassim Mbega au mwana Ukawa mwingine. Mbega aliyegombea mwaka 2005 na kuonyesha mvuto uliompa ushindi zaidi mwaka 2010 ni msomi mahiri aliyebobea kwenye masuala ya usimamizi wa hoteli na utalii na wakati huohuo akiwa mtaalam wa ufundishaji wa miradi mikubwa na midogo ya wajasiriamali na akifanikiwa kuifanya kazi hii kwenye maeneo mengi ya Jimbo la Mkinga. Pamoja na yote hayo itaipasa Ukawa kujipanga na kuwekeza kwenye jimbo la Mkinga, wananchi wanasema wanakosa matumaini na uongozi uliopo na wangehitaji kufanya mabadiliko. Jimbo hili ni jepesi kwa Ukawa lakini ni jepesi pia kwa CCM. Atakayemuwahi mwenzie kimbinu atalibeba bila ubishi. Ni suala la mipango tu.
JIMBO LA MUHEZA
Jimbo la Muheza linamiliki sehemu yote ya Wilaya ya Muheza likiwa na kata 34, vijiji 135 na vitongoji 522. Mkinga kuna watu 204,461 kati yao wanaume ni 204,461 na wanawake ni 100,843 na kuna wastani wa watu wanne kwa kila kaya.
Watu wengi wanaifahamu Muheza kwa sababu ukipita jimboni hapa ndiyo unaingia mkoani Tanga. Ni mahali palipochangamka kiasi na hata siasa zake zilianza uchagamfu tangu mwaka 1995. Jumla ya vyama 8 viliweka nia na ajabu ni kuwa vyama vitano vilikabana koo kama viko mbio fupi (Sprinting) huku vitatu vikichuana na kuachana kwa mbali na kutengeneza kundi lenye mshindi.
Vile vitano ni UPDP, UMD, TADEA, CUF na Chadema na vile vitatu ni NLD, NCCR na CCM. Wananchi wa Muheza wanasema upinzani ulikuwa na nafasi ya kuchukua jimbo hili mwaka 1995 lakini kusimamisha wagombea 7 kuligawanya kura na kufanya hata zile kura za ushindi za wapiga kura wanaochelewa kufanya maamuzi (undecided voters) wakaipigia CCM.
Vile vyama vitano vya kundi la “sprinting” kwa ujumla vikapata asilimia 20.7 akiwemo mwanajeshi mwingine mstaafu, Meja Jumaa Kichenje wa NLD – unaweza kudhani kuwa kulikuwa na mapigano ya kivita hapa! CCM ikashika uongozi ikimtanguliza Semwaiko.
Mwaka 2005 upinzani ulizidi kufifia, Muheza ikachanganyikiwa na kuchukua muda mwingi ikiimba na kutafakari ujio wa Kikwete ‘Chaguo la Mungu’ katika uchaguzi ambao ulipata wagombea ubunge sita na wanne kati yao wakiwa dhaifu huku mpinzani wa dhahiri (CUF) pia akiwa anajikongoja.
CCM ilimpitisha James Herbert kupeperusha bendera na CUF ikamtumia kada wake maarufu Abubakary Rakesh, mwanasiasa machachari na mtu mwenye upeo mkubwa na masuala ya uongozi. Rakesh pamoja na uwezo wake hakuweza kuitikisa CCM na aliishia kupata asilimia 12.9 (kura 7,841) na Mntangi wa CCM akazoa ushindi wa asilimia 85.4 (kura 52,065) na kuwa mbunge wa Muheza hadi mwaka 2010.
Mambo ya 2010 hayakutofautiana sana na 2005 japokuwa mara hii badiliko kubwa lilikuwa ni kuibuka kwa Chadema na kupungua kidogo kwa nguvu za CCM. Wagombea waliojitokeza ni watano, watatu kati yao wakiwa na uhai wa kushawishi wapiga kura. CCM ilimsimamisha James Herbert kwa mara ya pili akapata asilimia 75.77 (kura 34,836) akifuatiwa na Rakesh wa CUF aliyepata asilimia 12.92 (kura 5,938) na namba tatu ikaenda kwa Said Jumbe wa Chadema akipata asilimia 7.5 (kura 3,449).
James Herbert mwenye umri wa miaka 65 akiwa na shahada ya uzamili ya sayansi na uzoefu mkubwa wa kufanya kazi serikalini anakabiliwa na upinzani mkali ndani ya CCM ambapo kada mzoefu Adadi Omar anapewa nafasi nzuri ya kushinda kura za maoni ndani ya chama hicho.
Hata hivyo, mtandao wa upinzani siyo mzuri sana na mjenzi mkubwa wa Muheza na aliyekuwa mgombea 2005 na 2010, Abubakary Abdallah Rakesh alishaiaga CUF miaka kadhaa iliyopita akimfuata Hamad Rashid Mohammed na baadaye alijiunga na Chama cha ADC ambacho hakina mtandao Muheza.
Matokeo ya serikali za mitaa ya mwaka jana yanaonyesha CCM ikichukua asilimia 90.4 ya vijiji vyote na asilimia 89.2 ya vitongoji vyote 522. Hadi sasa CUF ina kada mmoja anayelimendea Jimbo la Muheza, Charles Erasto Mgaya, ambaye ni daktari wa mifugo na Chadema inao vijana watatu wanaoisaka Muheza, wanne hawa wakisubiria uamuziwa Ukawa juu ya jimbo hili.
Hali ya kisiasa ya Muheza si nzuri kwa upinzani na CCM inajua ina kazi kubwa ndani ya chama tu. Tathmini ya wazi inaonyesha mapambano mwezi Oktoba hayatakuwa makubwa pamoja na uwepo wa nguvu ya Ukawa, hili ni jimbo linalohitaji kujengwa sasa na kulichukua kirahisi 2020. Siasa ni hesabu za muda mrefu sana na Ukawa ikiwekeza bila kufanya ajizi inaweza kulitwaa kirahisi, lakini si Oktoba mwaka huu.
Leo tumekamilisha uchambuzi wa majimbo 11 ya Mkoa wa Tanga, Jumatano ya wiki ijayo (tarehe 01 Aprili) tutahamia Mkoa wa Shinyanga kwa kuanza kuchambua majimbo ya Shinyanga Mjini na Solwa.
Mwandishi na Mchambuzi
wa Makala hii ni Julius Mtatiro
(Julius Mtatiro ni
kiongozi mzoefu katika siasa. Ana shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi
(M.A), na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (L LB): +255787536759,
kuelekeamajimboni@yahoo.com – Uchambuzi huu ni maoni binafsi ya mwandishi).

No comments:
Post a Comment