Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa rais wa kwanza wa Tanzania, na mara nyingi
anatajwa kama "baba wa taifa". Kwa hakika aliiathiri kuliko yeyote
yule. Ndiye mwasisi wa itikadi ya ujamaa na kujitegemea iliyotangazwa hasa
katika Azimio la Arusha.
![]() |
|
Hayati Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere
enzi za Uhai wake
|
Kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa ni mwalimu. Kazi hiyo ndiyo
iliyompatia jina ambalo lilimkaa maisha yake yote la "Mwalimu."
Kwanza aliongoza Tanganyika toka mwaka 1961 hadi 1964
kama waziri mkuu, halafu kama rais; baada ya muungano wake na Zanzibar,
aliongoza Tanzania kuanzia mwaka 1964 hadi mwaka 1985 kama rais.
Mwalimu Nyerere ni kati ya viongozi wachache wa Afrika
ambao wameacha madaraka kwa hiari
baada ya kutawala kwa muda mrefu, akiwa bado anapendwa na wananchi walio wengi.
Alipostaafu urais mwaka 1985 alirudi kijijini kwake
Butiama ambako aliendesha shughuli za kilimo.
Hata hivyo aliendelea kuwa na athari kubwa katika siasa ya Tanzania hadi kifo
chake.
Kwa ruhusa ya makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani, Jimbo Katoliki la Musoma
linashughulikia kesi ya kumtangaza mwenye heri na hatimaye mtakatifu. Kwa sababu hiyo anaitwa pia "mtumishi wa Mungu".
Maisha Yake
Julius Kambarage Nyerere alizaliwa tarehe 13 Aprili mwaka 1922 katika
kijiji cha Butiama, wilaya ya Musoma, mkoa wa Mara, Tanzania (wakati ule: Tanganyika).Alikuwa
mmojawapo kati watoto 26 wa Nyerere Burito, chifu wa kabila
la Wazanaki.
Alipokuwa mtoto Nyerere alichunga mifugo ya baba
yake; katika umri wa miaka 12 aliingia shule
akitembea kilomita 30 hadi Musoma.Baada ya kumaliza shule ya msingi
aliendelea kusomea shule ya wamisionari Wakatoliki huko Tabora.Katika umri wa miaka 20 alibatizwa akawa Mkristo Mkatoliki hadi mwisho wa maisha
yake.
Mapadri wakiona akili
yake kubwa walimsaidia kusomea ualimu huko Makerere, Kampala, Uganda
kuanzia mwaka 1943 hadi 1945.Akiwa Makerere alianzisha tawi la Umoja wa
Wanafunzi Watanganyika, pia alijihusisha na tawi la Tanganyika African Association (TAA).Baada ya kumaliza masomo
ya ualimu alirudi Tabora akifundisha shule ya St.Mary.
Mwaka 1949 alipata udhamini wa masomo kwenda kusoma
kwenye Chuo Kikuu cha Edinburgh, Uskoti,
Ufalme wa Muungano,
akapata M.A. ya historia na uchumi (alikuwa Mtanganyika wa kwanza
kusoma katika chuo kikuu cha Uingereza na wa pili kupata shahada ya elimu ya juu nje ya
Tanganyika).
Aliporejea kutoka masomoni, alifundisha Historia, Kiingereza na Kiswahili katika shule ya St. Francis iliyo karibu
na Dar es Salaam.
Mwaka 1953 alichaguliwa kuwa rais wa chama cha
Tanganyika African Association (TAA), chama ambacho alikisaidia kukijenga
alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Makerere.
Mwaka 1954 alibadilisha jina la chama cha TAA kwenda
chama cha Tanganyika African National
Union (TANU), ambacho pia kilikuwa cha kisiasa zaidi kuliko TAA.
Ndani ya mwaka mmoja chama cha TANU kikawa tayari chama cha siasa kinachoongoza
nchini Tanganyika.
Uwezo wa Nyerere uliwashtua viongozi wa kikoloni akalazimika kuchagua kati ya siasa na kazi ya ualimu.
Nyerere alisikika akijisemea kuwa mwalimu kwa kuchagua na mwanasiasa kwa bahati mbaya.
Alijiuzulu ualimu na kuzunguka nchi nzima ya Tanganyika
kuzungumza na watu wa kawaida na machifu ili kuleta umoja katika kupigania uhuru.
Pia alizungumza kwa niaba ya TANU katika Trusteeship Council na Fourth
Committee ya Umoja wa Mataifa (UN) huko
New York.
Uwezo wake wa kuongea na wa kuunganisha watu ulimwezesha
kufanikisha Tanganyika kupata uhuru bila umwagaji wa damu.Ushirikiano
mzuri aliouonyesha aliyekuwa gavana wa wakati huo, Richard Turnbull,
ulisaidia pia kuharakisha upatikanaji wa uhuru.
Nyerere aliingia katika bunge
la kikoloni mwaka 1958 na kuchaguliwa kuwa waziri mkuu mwaka 1960.Mwaka
1961
Tanganyika ilipata uhuru wake na tarehe 9 Desemba 1961 Nyerere alichaguliwa kuwa waziri mkuu wa Tanganyika huru; mwaka mmoja baadaye akawa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika.
Nyerere alikuwa kiungo muhimu katika muungano wa Tanganyika
na Zanzibar kutengeneza Tanzania mara baada ya mapinduzi ya
Zanzibar mwaka 1964 yaliyomtoa madarakani sultani wa Zanzibar Jamshid bin
Abdullah.Tarehe 5 Februari 1977 aliongoza chama cha TANU
kuungana na chama tawala cha
Zanzibar Afro Shirazi
Party na kuanzisha chama kipya cha CCM (Chama cha Mapinduzi) akiwa
mwenyekiti wake wa kwanza.
Nyerere aliendelea kuongoza taifa
hadi 1985 alipomwachia nafasi rais wa pili, Ali Hassan Mwinyi.Aliacha kuongoza Tanzania ikiwa ni mojawapo
kati ya nchi maskini zaidi duniani, ingawa yenye huduma za elimu na afya
zilizoenea kwa wananchi wengi.
Hata hivyo aliendelea kuongoza CCM hadi mwaka 1990
na kuwa na athari kubwa katika siasa ya Tanzania hadi kifo chake.Kwa mfano,
inasadikika kuwa Nyerere alishawishi uteuzi wa Benjamin W.
Mkapa kama mgombea wa urais
mwaka 1995, ambaye alichaguliwa kuwa rais kwenye uchaguzi.
Nyerere alikaa muda mwingi kwake Butiama akilima shamba lake. Pamoja
na haya alianzisha taasisi yenye jina
lake; mwaka 1996 alionekana akiwa mpatanishi wa pande
mbalimbali za vita vya wenyewe kwa wenyewe
huko Burundi.
Tarehe 14 Oktoba 1999 aliaga dunia katika hospitali ya St Thomas mjini London
baada ya kupambana na kansa ya damu.
Mafanikio
Kati ya mafanikio makubwa ya Nyerere kuna: kujenga umoja
wa taifa kati ya watu wa makabila na dini tofauti, na hivyo kudumisha amani
ya muda mrefu tofauti na hali ya nchi jirani, iliyofanya Tanzania iitwe
"kisiwa cha amani".
Pia kustawisha utamaduni wa Kiafrika pamoja na lugha
ya Kiswahili, kushinda ubaguzi wa rangi, kutetea usalama wa taifa
katika vita dhidi ya mvamizi Idi Amin wa Uganda.
Kutoa mchango kwa vyama vya ukombozi vya nchi za
Kusini mwa Afrika kama
vile: Zimbabwe (ZANU), Afrika Kusini (ANC na PAC), Namibia (SWAPO), Angola
(MPLA) na Msumbiji (Frelimo).
Sifa zake
Pamoja na hayo, Nyerere bado anakumbukwa na Watanzania
hasa wa hali ya chini kutokana na sera zake za kujali utu.
Pia ataendelea kukumbukwa na Waafrika barani kote hasa kwa mchango wake mkubwa
wakati wa harakati za kupigania uhuru katika nchi mbali mbali barani Afrika.
Ni mmoja wa viongozi wachache waadilifu waliokwepa
kujilimbikizia mali pamoja na kutawala kwa miaka zaidi ya 24.
Mwishoni mwa maisha yake Nyerere aliishi kama mkulima wa
kawaida kijijini kwake Butiama. Alipatwa na kansa ya damu
(leukemia) akafariki Uingereza wakati wa kutibiwa katika mji wa London
tarehe 14 Oktoba 1999.

No comments:
Post a Comment