![]() |
|
DAVID Kafulila
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi)
|
Sheria hii ni muhimu
duniani kote na ndio maana hata Tanzania ilikuwa inangojea kupata sheria ya
kuongoza masuala ya mitandao yaani Cyber Law kutokana na uhalifu wa aina
mbalimbali wa masuala ya mitandao.
Sifa kuu ya sheria ya kuongoza masuala ya mitandao ni kuweka bayana
makosa ya mitandaoni na pia kuyatolea adhabu. Sheria hii inayopitishwa kwa
dharura madhara yake ni:
Moja, Kifungu 7 (2b): Mpokeaji wa ujumbe (receiver) anaweza kushtakiwa kwa
kosa la kupokea ujumbe ambao sheria imeufanya kuwa wa jinai. (Mfano: Mtu akikuforwadia
ujumbe, ukiupokea na wewe umefanya kosa la jinai).
Pili, Kifungu 21(1): Mtumia mtandao wa Intaneti yeyote hayuko salama kwani
mtoa huduma wake analazimika kutoa habari zake kwa serikali pale
zitakapohitajika (kwa lazima).
Tatu, Kifungu 8: Itakuwa ni kosa la jinai kama mtu ataweka wazi nyaraka za
siri za serikali hata kama ni nyaraka ya kusaidia nchi kwa ujumla (Mfano:
Matumizi mabaya ya mali ya umma).
Nne, Kifungu 14: Picha yoyote yenye mwelekeo unaoweza kuonekana kama ‘mchafu
kingono’ inaweza kupelekea mtu kufungwa hadi miaka 10 au kulipa milioni 30;
Sasa kama mtu kaweka picha yake Instagram ambayo sio ya ponografia lakini
‘ikatafsiriwa’ hivyo. Sheria haijatafsiri ponografia!
Tano, Kifungu 23: Je, ulijua kuwa ‘kusababisha maudhi ya hisia’ kwa mtu
mwingine ni unyanyasaji na unaweza kufungwa kifungo kisichopungua mwaka mmoja?
Sita, Rejea adhabu ya ibara mbalimbali: Sheria hii kila kosa linaweza fanya
mtu afungwe kifungo hadi cha maisha na kulipa pesa hadi zisizohesabika kwani hakijawekwa
kikomo cha juu cha adhabu bali kikomo cha chini tu kwa Kiingereza “not less
than”
Saba, Sheria haijaeleza vizuri suala la kutumia jina lisilo lako kwenye
mtandao na hivyo mtu anaweza kushitakiwa kama kuna mtu mwingine mwenye jina
kama hilo katika maisha halisi.
Nane, Serikali kupitia waziri husika ndio ina mamlaka ya kusema jambo
lililowekwa kwenye mtandao ni la kweli, uongo au la kupotosha. Kumbuka hata
ESCROW, EPA walisema ni uwongo; ni wangapi katika mtandao wangeshtakiwa
kiuonevu kwa hili?
Tisa, Kifungu 22: Ukiweka ujumbe katika mtandao na ukaufuta au kuuboresha,
kama ukishtakiwa kwa kuweka ujumbe huo unaweza kuhukumiwa pia kwa adhabu ya
kuuboresha au kuufuta. Ni mara ngapi unafuta ‘status’ zako za WhatsApp? Unaweza
shtakiwa kwa kuchelewesha ushahidi kisa tu ulifuta na hamna mtu anayeweza kujua
ulifuta kwa kusudi au la.
Kumi, Mkuu wa kituo cha Polisi chochote kile nchini anaweza kuagiza wewe
umpatie simu/laptop yako au taarifa zako zote (kwenye email, chats) au hata
vifaa vyako au ofisi yako kwa ajili ya upelelezi bila oda ya Mahakama.
Kumi na moja, Kifungu 31 (3a): “As soon as practicable” the law states. Askari
Polisi wakichukua vitu vyako wanaweza kukupatia listi ya vitu walivyovipokea
muda watakaoona kwao inawezekana kufanya hivyo. Jiulize, inaweza chukua muda
gani?
Kumi na mbili, Kifungu 31-35 & 39-45: Kama wewe ni Blogger au mtoa huduma ya
mtandao, pale unapobaini kosa ukalitoa na uko katika mikakati ya kuitaarifu
mamlaka husika (Kama sheria inavyosema), askari naye anaweza kwa wakati huohuo
akaja kukagua na kuchukua vitu vya kazi zako, hivyo sheria inakinzana yenyewe
kwa yenyewe. Blogger yuko sawa kisheria na askari yuko sawa kisheria.
Je, sheria hii ikisainiwa na Rais Jakaya Kikwete tutapona?
DAVID Kafulila
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi)

No comments:
Post a Comment