Ofisa wa Shirika la Equality for Growth (EfG),
Pauline Mdendemi akizungumza na wanawake wafanyabiashara masokoni katika
soko la Mchikichini Dar es Salaam jana kutoka Wilaya ya Lushoto ambao walifika
Manispaa ya Ilala kwa mafunzo ya siku tatu kuhusu mambo mbalimbali pamoja
na masuala ya vicoba.
|
Na Mwandishi Wetu.DSM
WANAWAKE
wafanyabiashara katika masoko wametakiwa kujenga tabia ya kutunza kumbukumbu
zao na kufanya vikao vya mara kwa mara jambo litakalosaidia kuwapunguzia
changamoto za kazi zao.
Mwito huo
ulitolewa na Ofisa wa Shirika la Equality for Growth (EfG), Pauline Mdendemi
wakati akizungumza na wanawake wafanyabiashara masokoni Dar es Salaam jana
kutoka Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga na Manispaa ya Temeke ambao wapo
Manispaa ya Ilala kwa ziara ya siku tatu ya mafunzo mbalimbali
pamoja na masuala ya vicoba yaliyofikia tamati jana.
“Jengeni
tabia ya kutunza kumbukumbu zetu pamoja na kufanya vikao vya mara kwa mara
itawasaidia kujua changamoto mlizonazo na kuzitatua ” alisema Mdendemi.
Mdendemi
alisema shirika hilo la EfG limefanikiwa kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa
programu ya “Sauti ya Mwanamke Sokoni” kwa Manispaa ya Ilala ambapo wanawake
wajasiriamali wameweza kupaza sauti ya kupinga vitendo vya kinyanyasaji
dhidi yao.
Alisema
shirika hilo lilifanya mradi wa miaka mitatu katika manispaa hiyo ambayo sasa
imekuwa ya mfano na ndio maana wafanyabiashara wanawake kutoka Lushoto mkoani
Tanga wamefika kujifunza ili nao elimu hiyo waipeleke kwa wenzao.
Alisema
lengo la mafunzo ni kuwapa fursa washiriki hao kuweza kujifunza kutoka kwa
wanawake wajasiriamali sokoni katika manispaa ya Ilala masuala mbalimbali
ikiwemo mbinu za kufanya ushawishi na utetezi ili kuboresha mazingira ya
ufanyaji kazi katika masoko.
Alitaja
malengo mengine kuwa ni namna ya kuongeza wanachama wa umoja na vicoba,
uendeshaji vikao vya umoja sokoni na namna mfumo wa kuweka na kukopa (Vicoba)
unavyoweza kuwasaidia wanawake wajasiriamali kukuza vipato vyao na kuboresha
biashara na maisha yao kwa ujumla.
Mdendemi
alitaja wajasiriamali walionufaika na mafunzo hayo kuwa ni wanawake wanne
kutoka wilaya ya Lushoto, Lukozi Lushoto watatu, Chamazi watatu na Temeke
Sterio watatu.
Mwenyekiti
wa soko la Lukozi kutoka Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Zakati Tendwa alisema
mafunzo hayo yamewafumbua macho kwani walikkuwa hawajui chochote kuhusu masuala
ya vicoba na kwa niaba ya wenzake amelishukuru shirika la EfG kwa kuwapigania
wanawake wajasiriamali masokoni.
No comments:
Post a Comment