Mto Zigi |
Wakaazi na wadau wa mazingira mkoani Tanga
wanaiomba serikali kuangalia uwezekano wa kutunga Sheria ya pamoja itakayoondoa
ukinzani uliopo ili kuimarisha usimamizi endelevu katika kuwadhibiti wavamizi wanaoharibu
chanzo cha maji cha Mto Zigi unaohudumia maelfu ya watu waishio jiji Tanga.
Wamesema utekelezaji wake utasaidia sana kuondoa
mwingiliano wa ki sekta unaosababishwa na udhaifu wa utekelezaji wa sheria
zinazosimamia rasilimali za maji pamoja na chanzo hicho kilichopo kijiji cha
Sakale na maeneo ya Amani katika wilaya ya Muheza.
Wametoa maoni hayo kwa nyakati tofauti katika
mahojiano na mRedio Huruma fm kuhusu namna bora ya kudhibiti shughuli endelevu
za uharibifu na uchafuzi zilizodumu kwa miaka 10 sasa kwenye chanzo hicho.
Maji ya Mto Zigi ambayo hujaza bwawa la Mabayani
kwa sasa ndiyo tegemeo pekee la chanzo cha maji ya kunywa kwa matumizi ya
wakazi 210, 435 pamoja na viwanda katika halmashauri ya jiji la Tanga.
Mratibu wa shughuli za Mazingira wa Mamlaka ya
Majisafi na Majitaka Tanga (UWASA), Ramadhani Nyambuka amesema kutokana na
uharibifu unaoendelezwa bila kikomo kwenye chanzo hicho ni vema sasa serikali
ikatunga Sheria ya pamoja itakayoweza kuwabana wahalifu.
Viongozi wa Bodi ya
Mamlaka ya Maji safi na Majitaka Mjini Tanga walipotembelea mto Zigi mwaka jana.
|
Naye Mhifadhi wa Hifadhi ya Mazingira Asili ya
Amani (ANR) Mwanaidi Kijazi amesema changamoto inayowakabili ni kukosekana kwa
sheria inayoweza kumbana mhalifu moja kwa moja hasa anapofikishwa mahakamani.
Ofisa Misitu wa Ofisi ya Katibu Tawala (RAS) mkoa
wa Tanga, Peter Nguyeye amesema kwa kuwa upo muunganiko wa moja kwa moja katika
masuala yanayohusu maji, mazingira na misitu ni vema sasa watunga sera wakaona
umuhimu na kutoa kipaumbele kwenye suala hilo.
Shughuli za uharibifu kwenye chanzo cha Mto Zigi
zinajumuisha kilimo cha mazao ya chakula na biashara ndani ya mabonde na kingo
za vijito kwa kutumia dawa za kuua magugu na wadudu, uchimbaji haramu wa
Dhahabu kwenye maeneo oevu, uvunaji wa miti mingi ya yote kwa wakati mmoja
kwenye msitu wa Longuza ili kupata magogo pamoja na uvuvi haramu.
No comments:
Post a Comment