POLISI
mkoani Tanga imesema imefanikiwa kupata bunduki aina ya SMG, ikiwa na risasi 20
ndani ya mapango ya Majimoto katika eneo la Amboni, inayodaiwa ilikuwa
ikitumiwa na wahalifu waliorushiana risasi na askari mwishoni mwa wiki.
Kamishna
wa Operation na Mafunzo ya kijeshi Paul Chagonja
|
Aidha,
imesema inashikilia watu kadhaa akiwemo aliyesababisha kupatikana kwa bunduki
hiyo. Baadhi ya watu wanaendelea kuhojiwa, kupata taarifa kwa lengo la kukamata
waliopora silaha kwa askari na kurushiana risasi kwenye mapango hayo.
Kupatikana
kwa silaha hiyo, kunafuatia msako maalumu uliodumu kwa siku nne sasa, uliolenga
kusaka silaha na wahalifu wanaodaiwa kujificha ndani ya mapango ya mawe
yaliyopo Amboni, nje kidogo ya mji wa Tanga.
Kamishna
wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja alitoa taarifa hiyo
jana kwa waandishi wa habari mjini hapa.
Alisema
mafanikio hayo, yametokana na subira ya wakazi wa Tanga na ushirikiano mkubwa
wanaoendelea kuuonesha kwa Polisi inayoshirikiana na vikosi vingine vya ulinzi
na usalama, kufanya operesheni ya pamoja kwenye eneo hilo.
“Kutokana
na taarifa kutoka kwa wananchi Februari 16 mwaka huu katika kitongoji cha la
‘Kona Z’ kilichopo Amboni, tulifanikiwa kumkamata mtu mmoja ambaye kwa sasa
sitamtaja jina kwa sababu upelelezi unaendelea, tulimhoji kwa kina akatupa
taarifa kuhusu silaha hii,” alisema.
Alieleza,
“Tulikwenda mpaka pangoni na kufanikiwa kupata SMG hii ikiwa na magazini moja
na risasi 20… silaha hii ni miongoni mwa zilizoporwa kwa askari mwezi
uliopita”.
Alisema
licha ya kupatikana kwa silaha hiyo, watu kadhaa wanashikiliwa wakihusishwa na
tukio hilo. Alisema upelelezi unaendelea kupata taarifa za kuwezesha kupatikana
kwa silaha nyingine na vitu mbalimbali vilivyowahi kuibwa.
“Naomba
wakazi wa Tanga na Watanzania kwa ujumla muendelee kuvuta subira na kutoa
ushirikiano…endelezeni utulivu na mshikamano kwa jeshi la polisi, ili kwa
pamoja tuweze kumaliza tatizo hili,” alisema.
Alisema
upo umuhimu mkubwa kwa wananchi, kuendeleza utulivu kwa kutokubali kuamini
taarifa potofu zenye kujenga hofu, zinazosambazwa na baadhi ya mitandao ya
kijamii kwa kuwa zinalenga kuwavuruga.
“Kimsingi
jeshi la polisi pamoja na vyombo vingine vya usalama, linaamini na kuthamini
kazi ya vyombo vya habari hasa vile makini, ambavyo vimeendelea kuwaarifu
wananchi habari sahihi ambazo hazina ghilba wala kuwachanganya”, alisema.
Alikanusha
taarifa zilizoenea mjini kwamba ipo miili ya wahalifu,iliyokutwa ndani ya
mapango hayo, kutokana na mapigano yaliyofanyika mwishoni mwa wiki.
“Ndugu
zangu mwanzoni tulikuwa tukisikia harufu kali ya kama miili iliyooza, kweli
tulijitahidi kutafuta na tukafanikiwa kuona mizoga ya ngedere na siyo binadamu
...wanyama hao walikuwa watatu na walikuwa na majeraha makubwa sana. Kwa hiyo
hawakuwa watu, bali ni ngedere ndio walikokuwa wamekufa na kuoza humo pangoni,”
alisema.
Akizungumzia
mkakati wa kupata silaha iliyosalia na vifaa vingine vilivyoporwa, Chagonja
alisema jeshi lake na kikosi cha operesheni hakitalala usingizi mpaka vitu
vyote vipatikane.
No comments:
Post a Comment