KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
imemfungia mechi tatu beki George Michael wa Ruvu Shooting kutokana na makosa
ya kinidhamu aliyoyafanya akiwa uwanjani.
Michael aliyelalamikiwa na TFF kwa kumkaba na kumchezea
kibabe mshambuliaji wa Yanga, Amisi Tambwe ambapo ni kinyume cha mchezo wa
kiungwana, ameadhibiwa kwa kuzingatia Ibara ya 48(1)(d) ya Kanuni za Nidhamu za
TFF Toleo la 2012. Alifika mbele ya Kamati hiyo juzi jijini Dar es Salaam.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Wakili Jerome Msemwa
alisema Michael alipopewa nafasi ya kujitetea, alikana kufanya kosa hilo na
kudai magazeti yametengeneza picha hizo.
TFF iliwasilisha ushahidi wa magazeti mawili ya Champion
na moja la The Guardian kwa kuzingatia Ibara ya 96(3) ya Kanuni ya Nidhamu ya
TFF Toleo la 2012. “Katika uamuzi wake, Kamati imesema kitendo cha George ni
kinyume cha kanuni ya mchezo wa kiungwana (fair play), na kuongeza kuwa kanuni
za TFF kwa makosa kama hayo ni dhaifu, hivyo kuagiza zirekebishwe ili ziweze
kuwa kali zaidi,” ilieleza taarifa ya TFF.
Adhabu ya beki huyo wa Ruvu Shooting imekuja siku
chache baada ya Kamati hiyo ya Nidhamu ya TFF kutoa adhabu ya kumfungia mechi
nane beki wa Mbeya City, Juma Nyosso kwa kumdhalilisha mshambuliaji wa Simba,
Elias Maguri wakati beki wa Azam FC, Aggrey Morris amefungiwa mechi tatu
kwakumpiga mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi katika mechi zao zilizofanyika
hivi karibuni.
Katika hatua nyingine, kamati hiyo, imetupa malalamiko
yaliyowasilishwa na TFF dhidi Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mara (FAM),
Mugisha Galibona, na Katibu wa Simiyu (SIFA), Emmanuel Sorogo.
Kwa upande wa Sorogo, Kamati imesema baada ya kupitia
vielelezo vya pande zote, hasa upande wa mlalamikiwa imeridhika hakushiriki
katika kumpiga refa kwenye mechi ya Kombe la Taifa kwa Wanawake kati ya
Shinyanga na Simiyu.
Badala yake aliyehusika ni Kocha wa Simiyu, Emmanuel
Babu ambaye tayari uongozi umeshachukua hatua dhidi yake kwa kumsimamisha kwanza
wakati akisubiri kufikishwa mbele ya Kamati ya Nidhamu ya SIFA.
Kwa upande wa Galibona ambaye ripoti za Kamishna na
refa zilionesha kuwa alishiriki kuhamasisha marefa kupigwa baada ya mechi ya
Ligi Daraja la Kwanza kati ya Polisi Mara FC na Mwadui FC, Kamati imesema
mlalamikiwa aliwasilisha vielelezo vinne kuthibitisha kuwa hakuhusika.
Kamati imekubaliana na ushahidi, na kutupa malalamiko.
Aidha, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imempiga faini ya Sh
600,000 au kifungo cha mwaka mmoja Katibu Mkuu wa Villa Squad, Mbarouk Kassanda
kwa kuhusika na uhamisho wa mchezaji Omari Ramadhan ambao haukufuata kanuni za
usajili.
Katika hatua nyingine, Klabu ya JKT Mlale imeamriwa
kuilipa African Lyon Sh 600,000 ikiwa ni ada ya uhamisho na fidia kwa kumtumia
mchezaji Noel Lucas kinyume cha taratibu kwenye mechi.
No comments:
Post a Comment