MAMLAKA ya Udhibiti wa
Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza kushuka kwa bei za mafuta ya aina
zote ikilinganishwa na toleo lililopita.
Akizungumza na waandishi
wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Bw. Felix Ngamlagosi,
alisema kushuka kwa bei hizo kumetokana na kushuka kwa bei za mafuta katika
soko la dunia.
Alisema bei za rejareja
kwa mafuta ya petroli yameshuka kwa sh.74 kwa lita sawa na asilimia 3.63,
dizeli sh. 62, sawa na asilimia 3.25 na mafuta ya taa sh. 54, sawa na asilimia
2.88.
Bei ya jumla kwa mafuta
ya petroli imeshuka kwa sh. 73.75 kwa lita sawa na asilimia 3.83, dizeli sh.
62.08, sawa na asilimia 3.44 na mafuta ya taa sh.54.34, sawa na asilimia 3.04.
Aliongeza kuwa, bei za
mafuta masafi zimepungua katika soko la dunia kwa petroli, dizeli na mafuta ya
taa Julai na Novemba, 2014 kwa dola za Marekani 249.
"Septemba 2014 hadi
Januari mwaka huu, bei za mafuta katika soko la dunia zimepungua kwa sh. 311
kwa lita...mafuta ya petroli na dizeli sh. 244, mafuta ya taa sh. 207 sawa na
punguzo la asilimia 16.13.
"Katika kipindi
hicho, thamani ya shilingi ya Tanzania imeshuka kwa asilimia nne ukilinganisha
na dola ya Marekani, bei ya mafuta katika soko la ndani ingepungua zaidi kama
thamani ya shilingi isingeendelea kupungua," alisema.
Alisema kwa mujibu wa
sheria ya mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea
kupangwa na soko ambapo EWURA itahamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei
kikomo.
Aliongeza kuwa, kampuni
za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta kwa bei ya ushindani ili mradi ziwe
chini ya bei kikomo na kuvitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei hizo
katika mabango yanayoonekana.
Alitoa wito kwa wanunuzi
wa bidhaa hizo kuhakikisha wanapata risiti ya malipo inayoonyesha jina la
kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.
CHANZO: MAJIRA
No comments:
Post a Comment