CHAMA cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewatimua wanachama wake 42 wakiwemo
wagombea walioshindwa kupita kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa hivi
karibuni.
Kwa
mujibu wa taarifa ya chama hicho, kutimuliwa kwa wanachama wake hao ni hatua ya
chama hicho kujisafisha kutokana na kile kinachodaiwa kwamba baadhi ya wagombea
hao wanatuhumiwa kufanya hujuma wakati wa mchakato wa uchaguzi serikali za
mitaa, vitongoji na vijiji uliofanyika Desemba 14, mwaka huu.
Akitangaza
uamuzi huo mjini humo, Katibu wa Chadema Jimbo la Korogwe Mjini, Ezekiel Mbwilo
alisema wahusika waliotimuliwa uanachama wanatuhumiwa kwa kukubali vitisho na
wengine kurubuniwa kwa fedha za wapinzani wao, hatua iliyowalazimu kwenda
kuondoa majina yao katika hatua za mwisho kuelekea kwenye kinyang’anyiro hicho.
“Tuligundua
kuwa baadhi ya wahusiska walijihusisha na hujuma mbalimbali dhidi ya chama
chetu, ikiwamo kukubali kupewa fedha na wapinzani wao ili wajiondoe. Tangu
awali, tulishakubalina kwamba ikibainika watu waliofanya hujuma tutawatimua
kundini na hapa ndipo tunahitimisha lile tulilokubaliana,” alisema.
Mbwilo
alitaja maeneo wanayotoka wanachama hao waliotimuliwa na idadi yao kwenye
mabano ni Kwamsisiwatu (6), Mahenge (10), Kitifu (25) pamoja na mmoja kutoka
Manundukati ambaye alidai kwamba mhusika huyo aliamua kujitoa kwenye
kinyang’anyiro cha uchaguzi ukiwa katika hatua za mwisho baada ya kurubuniwa na
wapinzani wa chama hicho.
Akizungumzia
vitisho alivyodai vilitolewa baadhi ya wanachama wa vyama vingine dhidi ya
wagombea wa Chadema, Mbwilo alisema tayari amewasilisha taarifa hizo kwenye
vyombo vya usalama na katika jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi.
No comments:
Post a Comment