![]() |
|
Aziza Hassani
akimuuguza mtoto wake Zuhura Rajabu(17) aliyelazwa katika Hospitali ya Wilaya
ya Handeni, baada ya kuungua mwili mzima walipokuwa wakifanyiwa dawa kwa mganga
wa kienyeji ambapo mama huyo alipata majeraha madogo kichwani. Picha na Rajabu
Athumani.
|
“Ama
kweli hujafa hujaumbika,” walisema walimwengu wakiwa na maana kubwa kwamba
tangu kuzaliwa hadi kufa hupitia au kukumbwa na mabadiliko mbalimbali, lakini
litakavyotokea au lini ni siri ya Mungu pekee.
Binadamu
anaweza kuzaliwa bila kasoro yoyote na kujijengea matumaini ya kutimiza malengo
yake bila wasi wasi, lakini akapatwa na mkasa utakaofuta ndoto zake zote.
Hivi
ndivyo ilivyotokea kwa msichana Zuhura Rajab mwenye umri wa miaka 17, ambaye
kwa mfumo wa maisha ya Kitanzania hajatimiza ndoto yake hata moja, awe akiishi
kijiji au mjini kwani hajafikisha umri wa kujitegemea.
Mbali
na ukweli huo, maisha na ndoto za Zuhura zimefifia ghafla baada ya kuingizwa na
babu yake kwenye imani iliyogharimu maisha yake na sasa anauguza majeraha
kutokana na kuungua moto huku wataalamu wakisema asilimia 72 ya mwili wake
umeathirika kwa moto.
Mkasa
uliomkuta Zuhura hataweza kuusahau maishani mwake kwani maelezo ya kitaalamu
yanaonyesha kuwa akipona, asilimia chache ya viungo vyake vitaweza kufanya kazi
kwa usahihi kwani majeraha ya moto husababisha ngozi kujikunja.
Ilivyotokea
“Mimi
na wanangu tuliitwa nyumbani, tulifika kwa mganga mimi, mama yangu mzazi pamoja
na watoto wangu wawili. Sisi ndiyo tuliingizwa kwenye shimo, ila baba hakuingia
bali alibaki juu na yule mganga. Hadi tukio linatokea, hakusogea kabisa kwenye
lile shimo.”
Ndivyo
anavyoanza kusimulia Aziza Hassani (35) mama wa watoto wawili ambaye yeye na
mtoto wake mmoja wamepona kwenye tukio hilo la moto uliowashwa kwa makusudi na
mganga wa kienyeji nao kuambiwa watoke huku moto ukiwaka na atakayeshindwa,
atakuwa amekamatwa na dawa ya mganga huyo.Anasimulia kwamba November 26
alipigiwa simu na mama yake mzazi aliyemweleza kuwa kuna dawa (tambiko) la
wanafamilia hivyo yeye na wanawe kutakiwa kwenda nyumbani kwa ajili ya shughuli
hiyo.
Anaeleza
kuwa alifika nyumbani mapema siku hiyo hiyo akiitika wito wa wazazi wake na
kuelezwa kwamba anapaswa kushiriki kwenye dawa kesho yake Novemba 27, agizo
ambalo alikubaliana nalo, lakini alipouliza ni dawa ya nini alielezwa kuwa ni
tambiko.
Aziza
anaeleza kuwa walifika kwa mganga huyo na kuanza kufanyiwa dawa iliyofanyika
ndani ya shimo ambalo liliezekwa kwa nyasi kavu juu yake na kuachwa nafasi
ndogo mfano wa mlango, ambao ndiyo walioutumia kuingilia ndani yake na dawa
ilifanyika.
“Mganga
alianza kufanya kazi yake sisi tukiwa ndani ya shimo. Tulikuwa mimi mtoto wangu
mdogo Hassan Rajab (4), Zuhura Rajabu (17) pamoja na mama yangu mzazi, Hadija
Abdallah(65) ambaye ndiye aliyeniita katika dawa hiyo,” anasema Aziza.
Anafafanua
kuwa iliwachukua zaidi ya nusu saa wakiwa ndani ya shimo hilo hadi hatua ya
mwisho ya dawa hiyo na walimwona mganga huyo akiwa amemaliza kufanya mambo yake
na kubaki pembeni ya shimo walilokuwamo.
Baada
ya muda walidhani mganga ameshamaliza na kumuuliza wanaweza kutoka, lakini
aliwajibu dawa bado inaendelea na ghafla mganga huyo aliwasha moto juu ya zile
nyasi.
“Moto
mkubwa ukaanza kuwaka ndipo mganga akatuamrisha tutoke shimoni huku moto
ukiendelea kuenea hadi mlangoni,” Aziza anasimulia kwa uchungu.
Anasema
kuwa baada ya kauli hiyo ya mganga kuwa waanze kujiokoa, alianza kumrusha nje
mtoto wake mdogo (Hassan) kisha kuanza harakati za kumsaidia mama yake na mtoto
wake mkubwa (Zuhura) lakini hakufanikiwa kutokana na moto kuwa mkubwa.
“Hivyo
mimi niliungua kichwani, mama yangu na mwanangu Zuhura miili yao ikaungua
vibaya,” anasimulia.
Anaeleza
kuwa baada ya moto kupungua, yule mganga na baba yake walikuja kuwasaidia
kuwatoa ndani ya shimo huku wenzake wakiwa wameshaungua kiasi cha kushindwa
kufanya lolote.
Baada
ya kutolewa majeruhi hao baba yake na mganga walimshauri wasipeleke majeruhi
hospitali wakawaeleza kuwa kuna daktari wao atakwenda kuwatibu katika kijiji
cha jirani na hapo walimhakikishia kuwa majeruhi hao watapona.
Hata
hivyo, Aziza anasema kuwa kwa daktari huyo hakuna kilichofanyika kwa zaidi ya
siku tatu na ilipofika Desemba mosi mama yake alifariki dunia hapo hapo
kijijini huku hali ya mtoto wake ikizidi kuwa mbaya kutokana na kukosa tiba.
“Kwa
huyo mganga hakuna tiba waliyopata zaidi ya kubandikwa pamba kwenye vidonda
vyao kwa siku zote tatu. Mama alifariki dunia kutokana na majeraha yake
kuendelea kila siku na maumivu makali,” anasema Aziza.
Anasema
kwamba jambo baya lililokuwa likiendelea kwa daktari huyo ni vidonda vya
majeruhi kuanza kuharibika na kutoa wadudu hali anayosema ilianza kumtisha
zaidi na kuanza kukata tamaa ya kupona.
Hospitali
Akizungumza
kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Handeni, Muuguzi Mfawidhi wa
Hospitali ya Wilaya ya Handeni Mwanaidi Semboja anasema kuwa walimpokea mgonjwa
huyo (Zuhura) akiwa katika hali mbaya huku vidonda vyake vikiwa havijapata tiba
yoyote.
Anasema
baada ya kumpokea walianza kumpa tiba za kitaalamu zaidi ikiwemo kumpunguzia
maumivu yaliyotokana na kuungua sehemu kubwa ya mwili wake hivyo kushindwa
kufanya lolote.
“Kwanza
tulianza kumpatia dawa za kumpunguzia maumivu kwani aliletwa akiwa kwenye hali
mbaya sana kutokana na kutofungwa vidonda. Kitaalamu ili kuzuia baridi,
tulianza kufanya hivyo na baada ya siku kadhaa mgonjwa aliendelea vizuri,”
anasema.
Muuguzi
huyo anasema kuwa kitaalamu binti huyo ameungua asilimia 72 na kwamba mgonjwa
kama huyo anatakiwa kuwa na uangalizi maalumu kwa muda wote.
Semboja
anasema kuwa wanawashukuru wasamaria wema waliotoa taarifa polisi ambao
walifika walipohifadhiwa majeruhi hao, kisha kuwachukua kuwapeleka hospitali,
ambapo yeye Aziza anaendelea vizuri, huku Zuhura akiendelea kupata tiba na
kuhamishiwa Hospitali ya Mkoa, Bombo mjini Tanga.
Wananchi
Aziza
Mkomwa mkazi wa wilayani Handeni anashauri akisema kuwa ni vyema wananchi
wakamrudia Mungu kwa kumwamini na kufanya ibada misikitini au kanisani, badala
ya kuendeleza imani potofu ikiwamo matambiko.
Anasema
ni muhimu kila mtu asimamie kwenye imani yake ya kidini kwa kufuata yale ambayo
vitabu vitakatifu vinamwongoza badala ya kwenda kinyume na maagizo ya Mungu
hata kukutwa na matukio ya ajabu kama yaliyomkuta Aziza na familia yake.
Polisi
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Tanga, Fraisser Kashai anathibitisha kutokea kwa tukio hilo
akisema kuwa mtuhumiwa amekamatwa na hatua zaidi kuchukuliwa.

No comments:
Post a Comment