MATUMIZI YA TIKETI ZA ELEKTRONIKI
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) iliyokutana jana (Desemba 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, imezingatia
upungufu uliopo katika utekelezaji wa matumizi ya tiketi za elektroniki.
Hivyo, Kamati hiyo imeiagiza Sekretarieti ya TFF kuwasiliana
na benki ya CRDB inayoendesha mfumo huo wa matumizi ya tiketi za elektroniki
kuhusu upungufu huo na kuhakikisha unafanyiwa kazi.
MAREKEBISHO YA KATIBA
YA TFF
Kamati ya Utendaji ya TFF imerejea mazungumzo kati yake na
ujumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) uliokuwa nchini
ukiongozwa na Meneja wa Vyama Wanachama wa FIFA, James Johnson.
Mazungumzo hayo kuhusu Katiba ya TFF yalifanyika Desemba 18
mwaka huu jijini Dar es Salaam
Kamati ya Utendaji inasubiri rasimu ya Katiba hiyo kutoka
FIFA ili iweze kufanya utaratibu wa kuwaarifu wanachama wake juu ya maudhui ya
rasimu hiyo.
Shughuli ya FIFA kurekebisha katiba za nchi wanachama wake
inaendelea duniani kote, na kwa Afrika kazi hiyo imekamilika katika nchi za
Namibia, Zimbabwe na Malawi.
USHIRIKIANO KATI YA
TFF NA SAFA
Kamati ya Utendaji imepitia na kupitisha makubaliano ya
ushirikiano kati ya TFF na Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA).
Makubaliano hayo ni ushirikiano katika nyanja za mpira wa
miguu wa vijana, maendeleo ya waamuzi, ufundi, menejimenti ya matukio (event
management) na utafutaji udhamini (sponsorship).
KANUNI ZA LESENI ZA
KLABU (CLUB LICENSING REGULATIONS)
Kamati ya Utendaji imejadili rasimu ya Kanuni za Leseni za
Klabu (Club Licensing Regulations), na kuagiza Kamati ya Sheria na Hadhi za
Wachezaji ifanye marekebisho ya mwisho, kabla ya kanuni hizo kusainiwa na
kuanza kutumika.
UANZISHAJI MFUKO WA
MAENDELEO YA MPIRA WA MIGUU (FDF)
Kamati ya Utendaji imepokea taarifa ya maendeleo ya mchakato
wa uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (Football Development
Fund- FDF).
Imeipongeza Kamati ya Mfuko huo inayoongozwa na Rais wa
zamani wa TFF, Leodegar Tenga, na kuitaka fanye jitihada za kukamilisha rasimu
ya kanuni za uendeshaji mfuko huo.
Mbali ya Tenga, wajumbe wengine wa mfuko huo ni Ayoub
Chamshama, Ephraim Mafuru, Frederick Mwakalebela, Tarimba Abbas na Zarina
Madabida. Sekretarieti ya mfuko huo inaundwa na Henry Tandau ambaye ni Katibu,
Wakili Emmanuel Muga na Boniface Wambura.
FDF ambao ni mfuko utakaokuwa unajitegemea utakuwa unashughulika
na maendeleo ya mpira wa miguu kwa vijana, na nyanja nyingine za maendeleo kwa
mchezo huo.
MKUTANO MKUU KUFANYIKA
SINGIDA MACHI 14
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) imepanga Mkutano Mkuu wa Kawaida wa mwaka ufanyike Machi 14 na 15 mwakani
mjini Singida.
MGOGORO NDANI YA ZFA
Kamati ya Utendaji imepokea kwa masikitiko taarifa za
masuala ya mpira wa miguu Zanzibar kupelekwa mahakamani.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) kitendo hicho ni kinyume cha taratibu za uendeshaji mpira wa miguu
ambazo zinakataza masuala ya mchezo huo kupelekwa katika mahakama za kawaida.
Kamati ya Utendaji inatoa rai kwa pande zote mbili
zinazohusika na mgogoro huo kukaa kwenye meza ya mazungumzo ili kumaliza
tofauti zao.
Kamati ya Utendaji imejitolea kutuma ujumbe wake Zanzibar
ili ukutane na pande zinazohusika katika mgogoro huo.
Ni muhimu usuluhisho upatikane haraka ili tuweze kujua hatma
ya washiriki wetu kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Imetolewa
Na
Shirikisho
La Mpira Wa Miguu Tanzania (Tff)

No comments:
Post a Comment