Mkoa wa Mara umeshika nafasi ya mwisho kitaifa katika
matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa mwaka 2014.
Aidha, wanafunzi 25,964 waliofanya
mtihani huo wamekosa nafasi ya kujiunga na elimu ya sekondari baada ya
kutofikia alama za ufaulu, licha ya shule ya kwanza kitaifa kutoka mkoani Mara.
Katibu tawala wa mkoa wa Mara,
Benedict Ole Kuyan, alisema hayo wakati akitangaza matokeo ya mtihani wa darasa
la saba na matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha
kwanza katika shule mbalimbali za sekondari, mwakani.
Kuyan
alisema licha ya shule ya msingi ya Twiboki wilayani Serengeti kushika nafasi
ya kwanza kitaifa kwa ufaulu, matokeo hayo hayakusaidia mkoa kufanya vizuri na
badala yake kujikuta ukishika nafasi ya 25 kati ya mikoa 25 ya Tanzania Bara.
Alisema
wanafunzi 18,385 wamechaguliwa kuingia kidato cha kwanza ikiwa ni asilimia 41.4
ya wanafunzi wote 44,349 waliohitimu elimu ya msingi mwaka huu, ukilinganisha
na asilimia 38.2 ya ufaulu wa matokeo ya mwaka 2013.
Aidha
wanafunzi 9,724 wameshindwa kumaliza elimu ya msingi kwa mkoa wa Mara kutokana
na sababu mbalimbali zikiwemo za vifo, utoro, mimba na uhamisho.
Katibu
tawala huyo, aliwataka wadau, wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla kukaa chini
na kusaidiana na serikali katika kulitafutia ufumbuzi wa haraka, tatizo la
kushuka kwa ufaulu.
Kwa
upande wake Afisa Elimu mstaafu wa mkoa wa Mara, Godon Mwita, alisikitishwa na
hali ya kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi wa shule za msingi na kuitaka serikali
kupitia wadau wa elimu kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.
Alisema
mkoa huo umeporomoka kutoka kumi bora kati ya miaka ya 80 hadi mwanzoni mwa
miaka 2000 na sasa kushika nafasi ya mwisho.
Chanzo: NIPASHE
No comments:
Post a Comment