MTANZANIA Charles Mihayo (36),
ambaye amechukua uraia wa Australia, amehukumiwa kifungo cha maisha jela, baada
ya kupatikana na hatia ya kuua watoto wake wawili wa kike Aprili mwaka huu.
![]() |
| MTANZANIA Charles Mihayo (36) |
Watoto waliouawa ni Savannah (4) na
Indianna (3), ambao Mihayo aliwaua kwa kuwaziba pumzi kwa mto wa kulalia. Vifo
vya watoto hao vimeacha simanzi kwani kwa mujibu wa Mihayo, alifanya ukatili
huo kutokana na chuki aliyonayo dhidi ya mama wa watoto hao, ambaye
ameshatengana naye kwa muda sasa.
Katika uchunguzi wa mauaji hayo
yaliyotokea Aprili 20, mwaka huu huko Melbourne, Australia, Mihayo aliwaambia
Polisi ilikuwa ni lazima afanye hivyo.
Siku ya mauaji Uchunguzi umeonesha
kuwa siku moja kabla ya mauaji, Mihayo alimtumia ujumbe mfupi wa simu mzazi
mwenzie akimuomba aone watoto wake kwa mara ya mwisho, na kumwambia kuwa
ameshinda.
Katika maandalizi ya kuona watoto
hao, ambao walikuwa wapelekwe nyumbani kwa baba yao, Mihayo aliwanunualia nguo
mpya na viatu na kisha walipofika kumuona baba yao, aliwavalisha na kucheza
nao. Wakati akicheza na malaika hao, Mihayo aliyekuwa akicheza na watoto wake,
aliamua kuwaua kwa kuwanyima pumzi kwa kutumia mto wa kulalia.
Baada ya mauaji Baada ya kufanikisha
unyama huo, Mihayo aliogesha miili ya watoto wake kisha akaivalisha nguo zao,
ndipo akapiga simu Polisi kutoa taarifa.
Hata hivyo, baada ya muda mama wa
watoto hao aliyekuwa nje ya nyumba hiyo akisubiri watoto wamalize kucheza na
baba yao, aliona kimya na ndipo akaenda kwenye mlango wa mzazi mwenzake na
kugonga na kujibiwa asubiri kidogo ataona.
Wakati huo Polisi walifika na
kugonga mlango na kisha Mihayo akafungua mlango huku akisema ‘nimeshamaliza,
nimewaua, nimeua watoto wangu’. Sababu, adhabu Polisi waliofika waliuliza kwa
nini ameua watoto wake na Mihayo alimuangalia mzazi mwenzie na kusema “muulizeni
huyu”.
Ila mwishowe aliwaambia askari
Polisi:”Hamtaelewa nini kinanisibu kufanya haya, na hata nikitoa sababu
haitasaidia,” alisema Mihayo. Baada ya mauaji hayo, familia ya mwanamama huyo
ilitoa tamko ikisema “hakuna adhabu ya kutosha au kifungo kinachoweza kuondoa
huzuni zetu kuhusu tukio hili, tutawakumbuka, na tuliwapenda sana hatutasahau”.
“Tunawashukuru wote wanaoendelea
kutufariji kwa sala na maombi katika kipindi chote kigumu, tunatoa shukrani
zetu kwa Polisi na maafisa washauri waliotusaidia,” lilisomeka tamko hilo.
Akisoma hukumu hiyo juzi, Jaji wa
Mahakama Kuu ya Victoria mjini Melbourne, Lex Lasry, alisema ukatili uliofanywa
na Mihayo ni tukio moja baya ambalo anapaswa kupewa adhabu ya kutumikia miaka
40 jela, na kisha kutumikia kifungo cha maisha.
Alisema ni lazima vyombo vya haki
vijifunze kupitia tukio hilo na kubainisha wazazi wenye roho za kikatili kama
hiyo ya Mihayo, ili kutoa ulinzi kwa watoto na kuepuka madhara kama hayo
yasitokee tena.


No comments:
Post a Comment