Dar Es Salaam
Imeelezwa kuwa maambukizi ya Virusi vya
Ukimwi (VVU), yanaweza kuongezeka nchini hasa kwa vijana kutokana na kubainika
kupungua kwa kasi ya matumizi ya mipira (kondomu).
Hayo yalielezwa jana na Katibu Mkuu, Ofisi
ya Waziri Mkuu, Dk Florens Turuka katika mkutano wa sita wa kutathmini
maambukizi ya VVU nchini.
Dk Turuka alisema maambukizi mapya
yameendelea kuwapo kwa sababu vijana hawatumii kondomu kujikinga.
“Matumizi ya kondomu katika jamii yamepungua
na kuwafanya watu wengi hasa vijana kupata maambukizi na zaidi ni kutokana na
mwamko mdogo kuhusu umuhimu wa kondomu kama kinga ya Ukimwi,” alisema.
Alisema utafiti uliofanyika mwaka jana
ulionyesha kuwa asilimia 50 ya waliojitokeza kupima VVU na kupata ushauri,
walikiri kutotumia kondomu. Hata hivyo, Dk Turuka alisema katika kipindi cha
miaka 10 iliyopita, maambukizi mapya yalipungua kutoka watu 180,000 hadi 72,000
kwa mwaka.
Alisema licha ya kuwapo mafanikio hayo,
kiwango cha matumizi ya kondomu kimeshuka na kuhatarisha maisha ya vijana wenye
umri kati ya miaka 15 – 39.
Alisema mwaka ujao wa fedha, Serikali
itaanzisha mfuko maalumu wa kukusanya fedha kwa ajili ya kununulia dawa za
kupunguza makali ya ugonjwa huo (ARV).
Alisema zaidi ya nusu ya wagonjwa
walioathirika wanahitaji dawa hizo.
Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya
Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Fatma Mrisho alisema wanafanya jitihada kuhakikisha
wanapunguza maambukizi mapya hadi kufikia sifuri ifikapo mwaka 2020.
Aliitaja baadhi ya mikoa yenye idadi kubwa
ya maambukizi mapya kuwa ni Njombe, Shinyanga, Mbeya, Dar es Salaam na Ruvuma.
“Katika miaka miwili ijayo, tutaelekeza
nguvu zetu kwenye mambo yanayochangia kuongezeka kwa maambukizi mapya, ikiwamo
maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kukabiliana na uhaba wa dawa,”
alisema.
No comments:
Post a Comment