Waziri
Mkuu Mizengo Pinda (pichani), amesema kuwa amesononeshwa na uamuzi wa wahisani
kuikatia Serikali misaada ya sh trilioni moja kutokana na kashfa ya IPTL.

Waziri
Mkuu Pinda, alitoa kauli hiyo , akijibu maswali ya papo kwa papo wakati wa
kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu bungeni.
Pinda,
alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Ole, Rajab Mbarouk Mohamed (CUF), aliyetaka
kujua sababu ya wahisani kukata misaada yao nchini na tamko la Serikali kuhusu
hali hiyo.
Akitoa
ufafanuzi zaidi wa swali hilo, Pinda alikiri wahisani wamekata misaada yao
nchini na mara nyingi wamekuwa na sababu zao mbalimbali, lakini safari hii
hatua hiyo imetokana na kashfa ya IPTL.
“Hawa
wahisani mara nyingi wamekuwa na sababu mbalimbali na hata huko nyuma
walishawahi kufanya hivyo, lakini safari hii wanasema wamekata misaada yao
kutokana na kashfa ya IPTL na wanasema wanasubiri ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ije, hili ni jambo linalonisononesha sana kwa
sababu uamuzi huo utaathiri watu wengi,” alisema Pinda.
Akitoa
msimamo wa Serikali kuhusu kashfa hiyo inayotikisa taifa, Waziri Mkuu Pinda
alisema bado hajakabidhiwa ripoti ya CAG na atakapoipokea, hatakuwa na sababu
ya kutoileta bungeni.
“Juzi
nilimsikia Waziri Lukuvi akisema Serikali haijaipata ripoti ya CAG. Kauli hiyo
ni kweli kabisa na nitakapoipata, sina sababu ya kukaa nayo,” alisema Pinda.
Hata
hivyo tayari Kamati ya Uongozi ya Bunge, imeagiza ripoti ya CAG ijadiliwe
katika mkutano huu wa Bunge Novemba 27 na 28 mwaka huu.
CHANZO:TANZANIA TODAY
No comments:
Post a Comment