TFF YARUDISHA LIGI DARAJA LA PILI
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana hivi karibuni imekubali mapendekezo
ya Kamati ya Mashindano ya kurejesha michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL).
Lengo la kurejesha ligi hiyo ni
kuongeza wigo wa mashindano kitaifa ambapo itasaidia kushirikisha kundi kubwa
zaidi la wachezaji kwenye mashindano makini yanayozingatia viwango na vigezo
ili kuwapa wachezaji maendeleo ya kiuchezaji ikiwemo kuendelezwa vipaji vyao
kitaalamu.
Ligi hiyo yenye timu 24 itachezwa
katika hatua ya makundi manne ya timu sita sita kwa mtindo wa nyumbani na
ugenini ambapo mshindi wa kila kundi atapanda kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Timu ya mwisho kila kundi itarudi kwenye ligi ya mkoa wake.
Hatua ya pili ni kutafuta bingwa wa
SDL ambapo timu zilizoongoza makundi (nne) zitacheza kwa mtoano nyumbani na
ugenini. Utakuwepo mchezo wa fainali ambapo mshindi atkuwa bingwa wa SDL msimu
wa 2014/2015.
Timu zitakazocheza SDL kwa msimu huu
ni zile zilizoshika nafasi ya pili hadi ya nane katika Ligi ya Mabingwa wa
Mikoa (RCL) katika makundi yao msimu uliopita, na tatu zilizoshuka kutoka FDL
msimu uliopita.
Kundi A litakuwa na timu za Milambo
FC (Tabora), Mji Mkuu FC (Dodoma), Mpanda United (Mpanda), Mvuvumwa FC
(Kigoma), Singida United (Singida) na Ujenzi (Rukwa). Kundi B ni Arusha FC
(Arusha), Bulyanhulu FC (Shinyanga), Eleven Stars (Kagera), Mbao FC (Mwanza),
Pamba FC (Mwanza) na Rwamukoma JKT (Mara).
Timu za kundi C ni Abajalo (Dar es
Salaam), Kiluvya United (Pwani), Kariakoo FC (Lindi), Mshikamano FC (Dar es
Salaam), Navy FC (Dar es Salaam) na Transit Camp (Dar es Salaam). Kundi D ni
Magereza FC (Iringa), Mkamba Rangers (Morogoro), Njombe Mji (Njombe), Town
Small Boys (Ruvuma), Volcano FC (Morogoro) na Wenda FC (Mbeya).
Ligi itachezwa kuanzia Novemba mwaka
huu.
FDL KUCHEZWA MAKUNDI MAWILI
Timu ya Ashanti FC inayoshiriki ligi Daraja la kwanza.
|
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa
2014/2015 itachezwa katika makundi mawili kwa mtindo wa nyumbani na ugenini
kuanzia Oktoba 11 mwaka huu.
Kundi A lina timu za African Lyon,
African Sports, Ashanti United, Friends Rangers, Kimondo SC, Kurugenzi Mafinga,
Lipuli, Majimaji, Mlale JKT, Polisi Dar es Salaam, Tessema FC na Villa Squad.
Wakati kundi B lina timu za Burkina
Faso, Geita Veterans SC, Green Warriors, Kanembwa JKT, Mwadui SC, Oljoro JKT,
Panone FC, Polisi Dodoma, Polisi Mara, Polisi Tabora, Rhino Rangers na Toto
Africans.
FIFA, TFF kutoa kozi ya ukufunzi wa utawala Desemba
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) wameandaa kozi ya ukufunzi wa utawala itakayofanyika Desemba mwaka huu.
Kozi hiyo itakayoendeshwa na
wakufunzi kutoka FIFA itafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Desemba 1 hadi 5
mwaka huu, ambapo sifa ya chini ya elimu kwa wanaotaka kushiriki ni kidato cha
nne.
Kwa wanaotaka kushiriki kozi hiyo
wanatakiwa kutuma maombi yao kwa Katibu Mkuu wa TFF. Mwisho wa kupokea maombi
hayo ni Septemba 12 mwaka huu ambapo wanatakiwa pia kuwasilisha nakala za vyeti vyao vya
kitaaluma.
Mbunge kufunga kozi za ukocha za CAF
Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Mheshimiwa Said Mtanda
|
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Huduma za Jamii, Mheshimiwa Said Mtanda anatarajia kufunga kozi ya ukocha ya
Leseni A ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) inayomalizika kesho
(Septemba 7).
Hafla hiyo ya ufungaji wa kozi hiyo
iliyoshirikisha makocha 22 itafanyika saa 7 mchana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu
ya Karume, jijini Dar es Salaam.
Kozi hiyo ya siku tano iliyokuwa
chini ya wakunzi wa CAF, Moatasim Mohamed Nasr kutoka Sudan na Sunday Kayuni wa
Tanzania.
No comments:
Post a Comment