Baadhi ya Watuhumiwa wa Kesi hiyo. |
RAIA wa
China waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya kuvua samaki kinyume cha sheria,
wamewasilisha barua kwa Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, kutaka
warudishiwe Meli ya Tawariq 1 na samaki waliopokewa mahakamani kama vielelezo.
Barua hiyo
iliwasilishwa na kampuni ya uwakili ya M and B iliyokuwa ikiwawakilisha Wachina
hao na kusaini na mshirika wa kampuni hiyo, Ibrahim Bendera.
Katika barua
hiyo, raia hao wanaiomba mahakama iwarudishie meli hiyo pamoja na tani 296.3 za
samaki zenye thamani ya Sh bilioni 2.074 ambazo zilipokelewa mahakamani hapo
kama vielelezo katika kesi namba 38/2009 iliyokuwa inawakabili.
Hatua hiyo
inatokana na amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyotolewa na Hakimu
Mfawidhi Isaya Arufani Agosti 23, mwaka huu wakati akiwaachia huru washitakiwa
wawili; nahodha wa meli hiyo, Hsu Chin Tai na wakala wa meli, Zhao Hanquing.
Awali watu
35 kutoka mataifa mbalimbali walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu na baadaye kesi hiyo ilihamishiwa katika Mahakama Kuu mbele ya Jaji
Razia Sheikh ambaye alipokea vielelezo hivyo.
Kesi hiyo
ilihamishiwa kwa Jaji Augustino Mwarija, ambaye aliwaachia huru washitakiwa 31
na kuwahukumu Tai na Hanquing kifungo cha miaka 30 jela au kulipa faini ya Sh
bilioni 22.
Hata hivyo
mmoja wa washitakiwa alifariki dunia wakati kesi hiyo ikiendelea. Washitakiwa
hao walikata rufaa kupinga adhabu hiyo.
Machi 28,
mwaka huu, Mahakama ya Rufani iliwaachia huru kabla ya kukamatwa tena na
kufunguliwa upya mashitaka hayo.
Wakati kesi
hiyo ikiendelea, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), aliwasilisha hati ya kutokuwa
na nia ya kuendelea kuwashitaki. Aliwaachia huru na Mahakama kuamuru
warudishiwe mali zao.
Washitakiwa
walikamatwa wakati Dk John Magufuli akiwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi, hali iliyochangia samaki waliokamatwa kuitwa wa 'Magufuli’ hasa baada ya
serikali kuamua kutaifisha meli na pia kugawa samaki kwa wananchi, vyuo na
taasisi nyingine za umma.
No comments:
Post a Comment