Na Mwanamichezo Wetu.TANGA
TIMU ya Coastal Union ya
Tanga “Wagosi wa Kaya” kesho Jumapili itacheza mechi ya kirafiki na
Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani ikiwa ni maandalizi ya
msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara ambao unatarajiwa kuanza Septemba 20 hapa nchini.
Akizungumza leo,Ofisa
Habari wa Coastal Union,Oscar Assenga amesema maandalizi ya kuelekea mchezo huo
yanaendelea vizuri na tayari walishafanya mazungumzo na uongozi wa wakata miwa
hao hivyo watawasili mkoani hapa siku moja kabla ya mchezo huo.
Assenga amesema kuwa mchezo
huo utakuwa ni wa pili kwa timu ya Coastal Union kucheza ikiwa mkoani hapa
baada ya kurejea kutoka Visiwani Pemba ilipokuwa imeweka kambi ya mwezi mmoja
kwa ajili ya matayarisho ya ligi kuu soka Tanzania bara.
Amesema baada ya mchezo wa
kwanza timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Polisi Morogoro hivyo
waliona umuhimu wa mechi hiyo lengo likiwa kukipa makali kikosi hicho kabla ya
kuwavaa wekundu wa msimbazi Simba siku ya ufunguzi wa Ligi kuu.
Ameongeza kuwa wanategemea
mechi hiyo itakuwa na upinzani mkubwa sana hivyo wakazi wa Tanga na vitongoji
vyake watumia fursa hii kuja kuiona timu yao ya Coastal Union ikipambana kwenye
mchezo huo kabla haijaanza msimu mpya wa ligi kuu Tanzania bara.
Hata hivyo amesema kuwa
msimu huu timu hiyo imepania kuhakikisha inafanya vizuri katika mechi zake za
nyumbani na ugenini ili kuweza kuchukua ubingwa wa Ligi kuu Tanzania bara.
No comments:
Post a Comment