Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Suleiman Kova |
JESHI la Polisi katika Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam, linawashikilia watu nane wanaotuhumiwa kuwa ni majambazi
sugu. Wawili kati yao wanahusishwa na tukio la kuuawa kwa Sista Cresencia
Kapuri (50) wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam katika Parokia ya
Makoka.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar
es Salaam, Suleiman Kova alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari,
jana.Alisema wahutuhumiwa hao, wakiwa katika utekelezaji wa uhalifu wao,
walisababisha vifo, majeraha, wizi wa mali na fedha taslimu.
Alisema watuhumiwa hao, walitumia
silaha za moto, ikiwa ni pamoja na bunduki aina ya SMG, bastola na vifaa
mbalimbali vya uvunjaji, ikiwa ni pamoja na baruti.
Alitaja watuhumiwa wanaohusishwa na
tukio la kuuawa kwa Sista Cresencia kuwa ni Manase Ogenyeka (35), maarufu kama
Mjeshi, mkazi wa Tabata Chang’ombe Manispaa ya Ilala, ambaye ni dereva wa
bodaboda ; na Hamisi Shaaban maarufu kama Carlos, mfanyabiashara, mkazi wa
Magomeni Mwembechai Manispaa ya Kinondoni.
Sista huyo aliyekuwa pia Mhasibu wa
Parokia ya Makoka na Mhasibu wa Shule ya Mwenyeheri Anwarite inayomilikiwa na
Kanisa Katoliki, aliuawa kwa kupigwa risasi Juni 23, mwaka huu katika eneo la
Riverside, Ubungo Kibangu, Dar es Salaam. Kova alisema licha ya kuhusishwa na
kifo cha Sista huyo, watu hao wanatuhumiwa kupora Sh milioni 20.
Alisema watuhumiwa hao, pia walikuwa
wakitafutwa kwa muda mrefu kwa tuhuma za uporaji wa Benki ya Barclays Tawi la
Kinondoni, uliotokea Aprili 28, mwaka huu, ambapo mamilioni ya fedha yaliibwa
kabla na baada ya tukio hilo.
“Jambazi Manase Ogenyeka ndiye
aliyeendesha pikipiki, akimbeba mwenzake akiwa na fuko la mamilioni ya fedha na
kutoroka nazo wakati Hamisi Shaaban ndiye aliyekuwa kiongozi katika tukio
hilo,” alidai Kova.
Mbali ya kuuawa kwa Sista Cresencia,
katika tukio hilo aliongozana na Sista Brigita Mbaga (32) na dereva wao, Mark
Mwarabu, aliyekuwa akiendesha gari aina ya Toyota Hilux Pick-Up, lenye namba
T213 CJZ ambaye alikatwa dole gumba lake kwa risasi baada ya kushambuliwa.
Alisema Jeshi la Polisi, bado
linawatafuta watuhumiwa wengine wawili katika tukio la kuuawa kwa Sista. Mtu
mwingine anayetafutwa ni Leonard Molel anayetuhimwa kwa tukio la wizi katika
Benki ya Barclays.
Kamanda huyo alisema watuhumiwa
wengine watatu, kati ya hao wanane, walikamatwa baada ya kutumia mbinu ya hati
bandia wakiwa wanaomba kazi katika kampuni binafsi ya ulinzi iitwayo Instant
Security Services Mtaa wa Makangira Msasani, Dar es Salaam.
Hao ni Elibariki Makumba (30) na
Nurdin Suleimani (40), wakazi wa Buguruni Madenge na Mrumi Salehe(38), mkazi wa
Kigogo Fresh.
Alitoa rai kwa kampuni za ulinzi,
yanapotaka kuajiri walishirikishe Jeshi la Polisi ili wafanye upekuzi wa
pamoja, utakaohusisha alama za vidole, picha na ukaguzi wa kumbukumbu muhimu za
kibayolojia kama vile vipimo vya DNA.
Aidha, aliwaomba wananchi ambao wana
tabia ya kutembea na fedha nyingi, kuacha kufanya hivyo, kwani kwa sasa
teknolojia imepanuka, hivyo kuweza kutumia simu za mkononi kuhamisha fedha
kutoka benki moja kwenda nyingine.
No comments:
Post a Comment