HII NI KWA MARA YA KWANZA JIJINI TANGA

HII NI KWA MARA YA KWANZA JIJINI TANGA
Tangaza biashara yako sasa uwafikie wateja wako kwa haraka na kwa gharama nafuu kupitia mfumo wa kisasa wa Digital Display Advertisement. Kupitia mfumo huu wateja wako watapata fursa ya kuona huduma zako na taarifa zote muhimu kupitia luninga kuwa za kisasa.

KIJIWE KIPYA CHA BURUDANI JIJINI TANGA

KIJIWE KIPYA CHA BURUDANI JIJINI TANGA
MPANGO MZIMA WA KULA BATA UKO HAPA

....HABARI NJEMA KWA AFYA YAKO...

....HABARI NJEMA KWA AFYA YAKO...
.....tumia fursa yako vizuri....

Tuesday, 22 July 2014

SAKATA LA MABAKI YA VIUNGO VYA BINADAMU LAFIKIA PATAMU "WAHUSIKA WAKAMATWA"


Makamu Mkuu wa Chuo cha International Medical and Technological University (IMTU), Profesa PV Prabhak Rao (mwenye koti la blue)  na viongozi wengine wakisindikizwa na polisi kuingia kwenye Kituo cha Oysterbay, Dar es Salaam jana, kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na upatikanaji wa viungo vya binadamu eneo la Mpigi Bunju. Picha na Rafael Lubava 


Wakati ikibainika kuwa viungo vya miili ya binadamu vilivyookotwa juzi katika Bonde la Mto Mpiji nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam vilitoka katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), jana Jeshi la Polisi liliwatia nguvuni watumishi wanane wa chuo hicho kuhusiana na sakata hilo.
Kukamatwa kwa watumishi hao kumeelezwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kuwa ni baada ya uchunguzi wa awali kubaini kuwa viungo hivyo kwa mara ya mwisho vilikuwa katika maabara ya IMTU.

Alisema tukio hilo lilitokea juzi jioni eneo la Bonde la Mbweni Mpiji ambako iligundulika mifuko ya plastiki 85 yenye mabaki ya viungo vya binadamu.
Kutokana na tukio hilo, Polisi imeunda jopo la wapelelezi saba likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu, Jafari Mohamed kusaidiana na daktari wa jeshi hilo kufanya uchunguzi wa miili hiyo.

“Katika uchunguzi wetu tulibaini kuwa hivyo viungo vya binadamu vilitolewa katika Chuo cha IMTU na kusindikizwa na mfanyakazi wa ngazi ya juu kwa ajili ya  kutupwa eneo la Bonde la Mbweni Mpiji,” alisema Kova.
Alisema mifuko hiyo ilikuwa myeusi ikiwa na viungo vya aina mbalimbali vikiwamo vichwa, miguu, mikono, moyo, mapafu, vifua na mifupa ya aina mbalimbali.

“Viungo hivyo havikuwa na harufu wala uvundo wa aina yoyote na vilionekana vimekaushwa na kukakamaa,” alisema.
Alisema katika eneo hilo walikuta vifaa vinavyotumika hospitali kama glovu, nguo maalumu (apron) 20 na karatasi mbili zenye maswali ya kujibu.
Kova alisema viungo hivyo vilichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Alisema jeshi hilo limefungua jalada la uchunguzi ili kujua sheria gani imevunjwa na kwa nini viungo hivyo vilitupwa hapo na kwa nini wasitumie utaratibu mzuri wa kuhifadhi na kwamba endapo kuna makosa ya kisheria, hatua zitachukuliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Muhimbili wapokea mabaki
Meneja Uhusiano wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema jana kuwa hospitali hiyo imepokea vifurushi 40 vyenye mabaki ya miili ya binadamu na kuhifadhiwa wakisubiri maelekezo ya polisi... “Hili ni suala la polisi, ninachoweza kusema ni kweli tumepokea vifurushi hivyo jana (juzi) usiku.”

IMTU yakiri kuhusika
Wakati Kova akisema hayo, uongozi wa IMTU ulikiri kuhusika na mabaki ya miili hiyo yaliyotupwa katika mto huo usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita.
Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Dk Fariji Mtango alisema jana kwamba anaamini miili hiyo inaweza kuwa ni ile iliyotoka katika chuo hicho, ambayo imekuwa ikifanyiwa mazoezi na wanafunzi kwa kuwa walihitaji kuiteketeza na walishatoa agizo hilo.

Alisema walitoa agizo kwamba mabaki hayo yapelekwe Muhimbili kwa mujibu wa utaratibu wao kwa kuwa hayakuwa na matumizi tena, kwa kuwa ndiyo sehemu yenye uwezo wa kuyateketeza na kutoa jukumu hilo kwa mmoja wa wakufunzi wa chuo hicho ambaye jana alikuwa safarini.
“Sasa zaidi hatujui kilichoendelea lakini tulipoangalia jana (Jumatatu) tulikuta sehemu yalipohifadhiwa imesafishwa, hivyo inawezekana ni sehemu ya vile vilivyoondolewa hapa. Hatukutarajia kwamba vingetupwa katika eneo lisilokuwa sahihi kama ilivyofanyika,” alisema.

Dk Mtango alisema hiyo ilikuwa moja ya hatua za kupisha wakaguzi ambao walitarajiwa kukuta maeneo yote ya kufundishia yakiwa katika hali ya usafi na unadhifu.

“Hawa wakaguzi wanapokuja wanatakiwa waone vitu vyote vikiwa sawa. Hata kama wangeona hayo mabaki ya miili ya binadamu isingekuwa tatizo, bahati nzuri wamekuja jana na wamefanya kazi yao vizuri,” alisema.
Muda mfupi baada ya kutolewa kauli hiyo, viongozi tisa wa chuo hicho na walinzi wawili walikamatwa mnamo saa 7.30 mchana na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay ambako wanashikiliwa, lakini baadaye Kova alisema waliokamatwa ni wanane.
Jana mchana eneo la chuo cha IMTU lilikuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi waliotanda kuanzia getini, mapokezi na kwenye bustani za chuo hicho na wengine waliovalia sare maarufu kama ‘tigo’ ambao walikuwa wakishika doria mbele ya chuo hicho.

Hatua kuchukuliwa
Dk Mtango alisema uongozi wa chuo hicho umeshtushwa na kutupwa kwa mabaki hayo katika utaratibu usiokubalika na utafanya uchunguzi na kuchukua hatua kwa wote waliohusika.
“Tunaanza na huyu ambaye tulimpa hili jukumu. Yeye ndiye aliyetakiwa kusimamia na anaujua wazi utaratibu wetu. Kwa sasa hajafika hapa na hata simu yake haipatikani. Tunaarifiwa kwamba amekwenda Zanzibar,” alisema.

Jinsi ilivyotokea
Juzi jioni, ilitokea taharuki baada ya wananchi kubaini viungo hivyo na taarifa kuanza kusambaa katika mitandao ya kijamii na baadaye vyombo vya habari na hadi jana mjadala kuhusu suala hilo ulikuwa mzito na wananchi wakihoji miili hiyo ni ya watu gani, imetoka wapi na imetupwa na watu gani.
Shuhuda wa tukio hilo, Mariam Nkumba alisema mara ya kwanza aliona mifuko yenye viungo hivyo Jumapili alipokwenda kuponda kokoto katika eneo hilo lakini hakubaini kulikuwa na nini.

Siku hiyo, Nkumba alisema aliondoka katika eneo hilo saa 12 jioni bila kujua nini kilikuwa ndani ya mifuko hiyo na siku iliyofuata (Jumatatu), alikwenda kuchukua mfuko mmoja ili ahifadhie kokoto zake, ndipo aliposhtuka kuona viungo vya binadamu.
“Mifuko ilikuwa mingi kweli, yote ilikuwa imejaa viungo vya binadamu. Mpaka sasa sijala na sina hamu ya kula. Ukiiona ile miili huwezi kula chakula,” alisema.

Mfanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi ya Skol iliyopo karibu na eneo hilo, Supery Kaijunga alisema mara alipopata taarifa kutoka kwa Nkumba alianza kutoa taarifa kwa wananchi wengine ili kwa pamoja wajue la kufanya.
Baadaye walitoa taarifa polisi ambao walifika saa mbili usiku na kukusanya mabaki yote na kuondoka nayo.
Hata hivyo, Kaijunga alieleza wasiwasi wake kuhusu wingi wa miili hiyo na kuhoji walikuwa watu gani na walitoka maeneo gani.
“Tukio hili siyo la kawaida na halijawahi kutokea huku kwetu. Tunakuwa na wasiwasi sana labda nasi maisha yetu yatachukuliwa kama hawa; polisi wafanye uchunguzi wa kina kubaini ukweli wake,” alisema Kaijunga.
CHANZO:MWANANCHI

No comments:

Post a Comment