Mh Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa itakayofanyika kitaifa katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki amesema kuwa maadalizi ya sherehe hizo yamekamilika na kuongeza kuwa maadhimisho ya mwaka huu kihistoria yanalenga kuwaenzi wote waliojitoa muhanga katika jitihada za kuikomboa ardhi ya Tanzania, kuilinda na kudumisha amani na utulivu uliopo.
Amesema maadhimisho hayo yatapambwa na shughuli mbalimbali zikiwemo Gwaride la Kumbukumbu litakaloonyeshwa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Ameongeza kuwa katika maadhimisho hayo kutakuwa na uwekaji na silaha za asili, maua kwenye mnara wa kumbukumbu pamoja na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini kutoa dua na sala kuliombea taifa.
Bw. Sadiki amefafanua kuwa shughuli zote katika viwanja vya Mnazi Mmoja zitaanza saa mbili Asubuhi na kumalizika saa sita mchana, pia wananchi watakaohudhuria kumbukumbu hiyo watapata fursa ya kushuhudia matukio yatakayokuwa yananendelea uwanjani hapo kupitia Luninga kubwa zitakazokuwepo katika maeneo yote muhimu ya uwanja huo.
Aidha, katika hatua nyingine ameeleza kuwa wakati wa maadhimisho hayo barabara ya Lumumba, Uhuru na Bibi Titi zitafungwa kwa muda kwa lengo la kuhakikisha usalama kwa watumiaji wa barabara hizo watakaohudhuria maadhimisho hayo.
No comments:
Post a Comment