Mkurugenzi wa TAKUKURU Dr. Edward Hosea, akizungumza na
waandishi wa Habari(Picha na Maktaba)
|
TAASISI ya kuzuia na kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mbeya, imemfikisha mahakamani Mhasibu wa Halmashauri
ya Wilaya ya Mbeya kwa kosa la kuhujumu uchumi na Rushwa.
Mtumishi huyo alifikishwa jana mbele
ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, James Mhanusi chini ya
Mwendesha mashtaka wa Takukuru, Nimrod Mafwele.
Mwendesha mashtaka wa Serikali Nimrod
Mafwele alimtaja mshtakiwa kuwa ni Geshon Bwile ambaye ni mhasibu wa
Halmashauri hiyo akituhumiwa kwa makosa matatu aliyoyatenda Mei 2, 2013.
Aliyataja makosa hayo kuwa ni pamoja
na kutumia Nyaraka za Serikali kujipatia fedha kinyume cha kifungu cha 22 cha
Sheria ya Takukuru namba 11 ya mwaka 2007.
Alisema katika kosa hilo Mtuhumiwa
akiwa ni mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya alitumia risiti yenye namba
0009 kumwandikia Rich & Mr&Mrs Mufat Decoration kwa malipo ya mapambo
yenye thamani ya shilingi Milioni 1,350,000 wakati sio kweli.
Mwendesha mashtaka huyo alilitaja kosa
lingine kuwa ni Ubadhilifu kinyume cha kifungu cha 28(1) namba 11 cha
mwaka 2007 ambapo alijipatia kiasi cha shilingi Milion 1,350,000
alichokabidhiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.
Alilitaja kosa la tatu kuwa ni
kuisababishia hasara mamlaka kinyume cha Sheria kifungu cha
10(1),(i),57(1) na 60(2) ya uhujumu uchumi namba 200 iliyofanyiwa marejeo mwaka
2002, ambapo Halmashauri ilipata hasara ya shilingi Milion 1,350,000 mali ya
Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Baada ya kusomewa mashtaka yote hayo
Mtuhumiwa alikataa yote ambapo upande wa mashtaka ulisema upelelezi umekamilika
na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kusikiliza maelezo ya awali.
Aidha mshtakiwa aliachiwa kwa dhamana
baada ya kukamilisha masharti ambayo ni kuwa na wadhamini wawili ambao ni
watumishi wa Serikali wakiwa na barua kutoka kwa mwajiri,mali kauli ya Shilingi
Milioni Moja kila mmoja.
Hakimu Mhanusi alisema mashariti
mengine ni kutokana na kifungu cha 148 (6) ambapo mtuhumiwa harusiwi kutoka nje
ya Mkoa wa Mbeya bila ruhusa ya mahakama pamoja na kuwasilisha hati ya
kusafiria kwenye kituo cha polisi jambo ambalo aliyatimiza papo hapo.
Hata hivyo kesi hiyo iliahirishwa hadi
Julai 25 mwaka huu ambapo mtuhumiwa ataanza kusomewa maelezo ya awali na
kuendelea kusikiliza upande wa mashahidi.
Kesi hiyo ni ya pili kwa TAKUKURU Mkoa
wa Mbeya kuwafikisha Mahakamani watumishi wa Halmashauri ya Mbeya baada ya hivi
karibuni kumfikisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Upendo Sanga,
na Watumishi wengine kwa kosa la kuhujumu uchumi.
No comments:
Post a Comment