Kamati ya Rufani ya
Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeikataa rufani ya
Michael Wambura kupinga kuenguliwa kugombea urais katika uchaguzi wa klabu ya
Simba unaotarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu.
Wambura aliwasilisha
rufani yake mbele ya Kamati hiyo iliyokutana jana (Juni 20 mwaka huu) jijini Dar
es Salaam chini ya Kaimu Mwenyekiti Wakili Mwita Waissaka kupinga uamuzi wa
kumwengua katika kinyang’anyiro hicho uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba
kwa kufanya kampeni kabla ya muda uliopangwa.
Baada ya kupitia
vielelezo, kanuni na sheria, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF imeridhika
kuwa mrufani (Michael Wambura) alifanya kampeni kabla ya muda kinyume na Ibara
ya 6(1)(a) na (g), Ibara ya 6(1)(l) pamoja na Ibara ya 14(3) ya Kanuni za
Uchaguzi za TFF toleo la 2013.
Kwa mujibu wa ibara
hizo, Kamati ya Uchaguzi ya Simba inayo mamlaka ya kumwengua (disqualify)
mgombea anayefanya kampeni ama kukiuka maagizo halali ya Kamati ya Uchaguzi.
Kamati ya Rufani ya
Uchaguzi ya TFF imeziagiza kamati zote za uchaguzi za wanachama wa TFF kufuata
kanuni za uchaguzi kama zilivyoainishwa katika Katiba zao ili kuepusha rufani
za mara kwa mara.
Uamuzi wa Kamati ya
Rufani ya Uchaguzi ya TFF umezingatia Katiba ya TFF pamoja na kanuni zake, na
pia Katiba ya Simba.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA
MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA
WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment