![]() |
|
Waziri wa Nishati na
Madini Profesa Sospeter Muhongo akimsikiliza Mkurugenzi Mkazi wa Mradi wa
ujenzi wa kituo cha Kinyerezi I, Bw. Shaun Moore, wakati akimweleza maendeleo
ya ujenzi wa kituo hicho.
|

![]() |
|
Mmoja wa mitambo ya
kufua umeme ambao utafungwa katika eneo la Kinyerezi I mara baada ya ujenzi
kukamilika. Mitambo hiyo, inatarajiwa kuzalisha kiasi cha megawati za umeme 150
ambazo zitaunganishwa katika gridi ya Taifa.
|
![]() |
|
Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Uwekezaji Mhandisi Decklan Mhaiki
(katikati) akimweleza Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter
Muhongo (kushoto) pamoja na Waandishi wa habari moja ya mashine za kufua
Umeme zitakazofungwa katika eneo la Kinyerezi I jijini, Dar es Salaam.
Kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa Mradi wa ujenzi huo, Bw. Shaun Moore
|
a Asteria Muhozya na Jema Marko, Dar es Salaam
Megawati
150 zinatarajiwa kuongezeka katika gridi ya Taifa mara baada ya kukamilika kwa
ujenzi wa mitambo ya kufua umeme eneo la Kinyerezi I pamoja na kukamilika kwa
ufungaji wa mitambo hiyo, ambapo shughuli zima inatarajiwa kukamilika kabla ya
mwezi Disemba mwaka 2014.
Waziri wa
Nishati na Madini Sospeter Muhongo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa
kituo hicho alieleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa kituo
hicho ni hatua mojawapo ya kutimiza azma ya Serikali ya
kuongeza umeme katika gridi ya Taifa.
Aidha,
aliwataka watanzania na wateja wa umeme kujenga imani na Shirika la Umeme
Tanzania kutokana na mabadiliko ambayo tayari yamefanyika katika shirika hilo
ikiwemo utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kuhakikisha kunakuwa na umeme wa
uhakika.
“Nataka
Watanzania muelewe kuwa, Tanesco ya sasa sio kama ya zamani. Umeme utapatikana.
Kampuni ya Jacobsen Elektro ambao wanafanya kazi ya ujenzi ni wazoefu katika
shughuli hizi, tuna imani kazi itakwenda vizuri kama tulivyopanga. Tanesco
itatatua tatizo la umeme”. Alisema Waziri Muhongo.
Katika
hatua nyingine, Profesa Muhongo alieleza kuwa, asilimia 98 ya
kampuni za kitanzania kupata kandarasi katika ujenzi huo ni fursa
mojawapo ambazo watanzania wanatakiwa kuzitumia katika kipindi hiki ambacho
nchi inaingia katika uchumi wa gesi.
Akizungumzia
kuhusu fedha za ujenzi wa kituo cha kinyerezi I na ujenzi wa vituo vingine vya
kinyerezi II, III na IV, Waziri Sospter Muhongo alieleza kuwa,
fedha za ujenzi wa kituo cha Kinyerezi I zimetolewa na Serikali kupitia
TANESCO. Ujenzi wa kituo cha kinyerezi II fedha itatokana na ubia
kati ya Serikali ya Tanzania na Japani , wakati ujenzi wa kinyerezi III na IV
fedha zitatokana na kuingia ubia kati ya Serikali na kampuni ya Kichina.
Wakati huo
huo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Uwekezaji, wa Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) Mhandisi Decklan Mhaiki, aliongeza kuwa, katika kituo hicho
zitafungwa jenereta nne ambapo kila moja itakuwa na uwezo wa kuzalisha kiasi
cha megawati 37.5, hivyo kufanya jumla ya megawati 150 kutoka kituo hicho.
Vilevile,
alieleza kuwa, katika jitihada za kuhakikisha kwamba Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) linatatua tatizo la Umeme nchini, tayari shirika hilo na mkandarasi
anayejenga kituo hicho, kampuni ya Jacobsen Elektro wameanza mazungumzo ili
kuongeza kiasi kingine cha megawati 200 ili kituo cha kinyerezi I kiweze kuzalisha
umeme wa kiasi cha megawati 350.
Akielezea
kuhusu ubora wa jenereta zitakazofungwa kituoni hapo, Mhaiki alieleza kuwa,
generator hizo ni za kisasa na hazina athari za kimazingira ikiwemo kelele.
Kwa upande
wake Mkurugenzi Mkazi wa Mradi huo kutoka kampuni ya Jacobsen Elektro,
Bw. Shaun Moore, akielezea maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho, alieleza
kuwa, ujenzi wa kituo hicho unaendelea vizuri kutokana na kampuni hiyo kufanya
kazi kwa ushirikiano mzuri na kampuni za kitanzania zilizochukua kandarasi
tofauti tofauti za ujenzi wa kituo hicho, ambapo takriban asilimia 98 ya
kandarasi na wafanyakazi ni kutoka kampuni za kitanzania.



No comments:
Post a Comment