![]() |
|
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Mecki Sadiki
akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kutoa agizo
kwa viongozi na watendaji wa jiji la Dar es salaam kuhakikisha kuwa wanawaondoa
na kuwachukulia hatua za kisheria wanaovunja sheria za jiji kwa kuendesha
shughuli mbalimbali katika maeneo yasiyoruhusiwa.
|
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar es salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Mecki Sadiki
amewaagiza viongozi na watendaji wa jiji la Dar es salaam kuhakikisha kuwa
wanawaondoa na kuwachukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha
mahakamani wakazi wa jiji la Dar es salaam wanaovunja
sheriaza jiji kwa kuendesha shughuli mbalimbali katika maeneo
yasiyoruhusiwa.
Aidha amewataka waendesha pikipiki maarufu kwa
jina la “Bodaboda”, Bajaji, waendesha baiskeli na mikokoteni wanaofanya
biashara ya kubeba abiria na mizigo maeneo yasiyoruhusiwa kisheria kuondoka
wenyewe kabla hatua kali za kisheria hazijachuliwa dhidi yao.
![]() |
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es
salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Mecki Sadiki amesema kuwa
jiji la Dar es salaam limeamua kuchuakua uamuzi huo kufuatia tatizo la baadhi
ya wananchi kuamua kuvunja sheria zilizowekwa kwa kisingizio cha ugumu wa
maisha na kutafuta fedha hali inayoleta usumbufu kwa wananchi wengine .
Amesema kuwa licha ya changamoto inayolikabili jiji
la Dar es salaam hasa maeneo ya katikati ya mji hali iliyopo sasa ya biashara
holela na uvunjifu wa sheria unaofanywa na maendesha Bodaboda, Bajaji,
baiskeli, mikokoteni na Taxi bubu maeneo yasiyoruhusiwa kisheria hauwezi
kuvumilika.
“Jiji la Dar es salaam tumekuwa na kero ya muda
mrefu hasa ya omba omba, waendesha baiskeli, bodaboda na wafanyabiashara katika
maeneo ya makutano ya barabara katika maeneo yasiyoruhusiwa hali hii hatuwezi
kuivulimia, sisi hatufukuzi watu bali tunawataka wafuate sheria za jiji”
Amesisitiza.
Ameeleza kuwa serikali haina lengo la kuwazuia
wananchi kufanya biashara na shughuli nyingine za kujiingizia vipato kama
wanazingatia sheria na taratibu zilizowekwa na kuongeza kuwa wale wote
wanaoomba leseni za kufanyia biashara wanapewa taratibu na miongozo na masharti
ya kuzingatia wanapofanya biashara zao jambo ambalo wengi wao wanashindwa
kulizingatia.
“Kila Manispaa ina miongozo na kanuni za uendeshaji
wa shughuli zake ikiwa ni pamoja na mamlaka ya kutenga maeneo ya biashara na
kuwaruhusu wale wanakidhi masharti ya leseni zao kufanya biashara zao ila wengi
wao hasa madereva wa Bajaji na Bodaboda hawazingatii haya” Amesisitiza Mh.
Sadiki.
Ameeleza kuwa sheria zote zilizotungwa zimewekwa ili
zifuatwe kwa ustawi wa taifa na si vinginevyo na kubainisha kuwa wote
waliovamia maeneo ya vituo vya mabasi, maeneo ya vituo vya umeme na hifadhi za
barabara ni vema wakaondoka wenyewe na kukubali kutii sheria bila shuruti huku
akitoa mfano wa baadhi ya wafanyabiashara na wauza vyakula “mama lishe” walio
anza kuvamia maeneo ya ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo Kasi (DART).
“Haiwezekani sheria za jiji zikavunjwa na sisi
tukaendelea kuwaangalia baadhi yao wamefikia hatua ya kuvamia maeneo ya mradi
wa mabasi yaendayo kasi na kuanza kufanya biashara na kuwasumbua mafundi jambo
lisilokubalika”
Akizungumza kuhusu biashara ya bodaboda inayofanywa
na vijana walio wengi jijini Dar es salaam Mh. Sadiki ameeleza kuwa mpango wa serikali
kuruhusu Bodaboda na Bajaji kutumika kubebea abiria ulikuwa na maana nzuri ya
kuwawezesha wananchi kupata usafiri hasa katika maeneo yasiyofikika kirahisi
kwa magari hasa vijijini na kuongeza kuwa utakua na mafanikio kama watafuata
sheria.
‘Serikali iliruhusu usafiri wa Pikipiki na Bajaji
kutumika kubebea abiria kwa nia nzuri ikiwa ni pamoja na kurahisisha usafiri na
kuongeza ajira,hivyo siyo nia yetu kuwadhalilisha vijana hawa tunachowataka
wafanye ni kufuata sheria za nchi”
Aidha kwa upande wa ongezeko la ombaomba ambao
baadhi yao walirudishwa katika maeneo yao ya awali na kurejea tena jijini Dar
es salaam ameeleza kuwa utaratibu wa kuwafuatilia uko pale pale na kufafanua
kuwa watakaokutwa na makosa ya kukaa maeneo yasiyoruhusiwa watafikishwa mahakamani.
Kwa upande wake Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es
salaam Kamishna (CP) Suleiman Kova ameeleza kuwa ni wakati sasa wa wakazi wa
jiji la Dar es salaam hususan madereva wa bodaboda na Bajaji kufuata sheria na
kusisitiza kuwa ni vema wananchi wakajenga mazoea ya kufanya tathmini ya safari
zao iwapo wanakidhi vigezo vya kuwawezesha kutembea barabarani.
“Kwa waendesha pikipiki “bodaboda” hali ni mbaya
wengi wameumia na kupata ulemavu wa kudumu kwa kutozingatia sheria za
usalama barabarani na kukidhi matakwa ya kuendesha pikipiki hizo”
Amesema kuwa Jeshi la Polisi litafanya kazi yake kwa
kushirikiana na manispaa zote tatu kuhakikisha kuwa vitendo vya uvunjifu wa
sheria vinakomeshwa na kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona
dalili zozote za uvunjifu wa amani hasa matukio ya ujambazi kwa kutumia
pikipiki yayoendelea kuongezeka kwa kasi.
“Napenda niwahakikishie wananchi kuwa jeshi la
polisi tumejipanga vizuri kukabiliana na vitendo vyote vya uhalifu wa aina
zote, pia natoa wito kwa wakazi wa jiji la Dar es salaam hasa wafanyabiashara
kuepuka kutembea na fedha nyingi ili kuepuka madhara ya kuvamiwa”
Naye Afisa Mfawidhi wa SUMATRA Kanda ya Mashariki
Bw. Conrad Shio ameeleza kuwa sheria ya usafirishaji kusimamia Bajaji na
Bodaboda iko wazi na kuongeza kuwa serikali ina wajibu wake na pia waendesha
pikipiki na Bajaji wanawajibu wao wa kuzingatia kanuni taratibu na kanuni
zilizowekwa.
“Sisi kama SUMATRA tunaendelea kufanya kila tuwezalo
kukabiliana na vitendo vyote vya uvunjivu wa sheria za barabarani”


No comments:
Post a Comment