Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani 'Profesa Majimarefu' |
SHIRIKA
la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), limempatia Mbunge wa Jimbo la Korogwe
Vijijini, Stephen Ngonyani 'Profesa Majimarefu' kiasi cha shilingi milioni 253
kwa ajili ya kukabili tatizo la maji katika jimbo lake fedha ambazo zimetokana
na mfuko wa maendeleo vijijini.
Akikabidhi mkataba wa fedha hizo, Ofisa Miradi Shirikishi wa UNDP, Stela Zaarh
amesema fedha hizo wamezitoa kwa wilaya hiyo kama jitihada za shirika hilo
kusaidiana na Serikali kutatua kero zinazowakabili wananchi vijijini hasa suala
la maji, afya na elimu.
Baada ya kupokea mkataba huo ambao fedha tayari zimeshaingizwa katika akaunti ya halmashauri ya wilaya kupitia mhandisi wa maji wa wilaya, mbunge huyo alisema kwamba fedha hizo zitachimba visima virefu katika vijiji vitano kata Majengo kilichopo kata ya Mswaha-Darajani, Makuyuni, Kikwazu, Goha na Kwetonge.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Lucas Mweri aliyekuwepo kwenye makabidhiano hayo amesema mchakato wa kuwapata wakandarasi watakaochimba visima hivyo utaanza mara moja na kwamba sasa hivi hatua za awali za kuandaa mapendekezo ya mradi huo utaanza wiki ijayo.
Mkuu wa wilaya Korogwe, Mrisho Gambo aliyekuwepo pia kwenye hafla hiyo ya kukabidhi mkataba huo alimtaka mkurugenzi huyo kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kufika kwa walengwa ili kuondoa kero ya maji kwa wananchi na pia kuwashawishi waliotoa fedha hizo kutoa fedha nyingine.
No comments:
Post a Comment