WATU sita
wamefariki dunia na wengine watatu kuokolewa katika boti ya abiria ya MV
Kilimanjaro iliyokumbwa na dhoruba ya mawimbi makali kutokana na kuchafuka kwa
hali ya hewa baharini.
Ajali hiyo
ilitokea jana katika eneo la mkondo wa Nungwi wakati boti hiyo ikitoka Pemba
kurudi Unguja.
Naibu Waziri wa
Mawasiliano na Miundombinu, Issa Haji Ussi alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo
ambapo watoto watatu wamefariki dunia pamoja na wanawake watatu wenye umri kati
ya miaka 36-50.
Kamishna wa
Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame alithibitisha ajali hiyo na kusema
uchunguzi zaidi unafanywa. Inadaiwa baada ya kuchafuka kwa bahari, wimbi moja
lilipiga sehemu ya mbele ya boti na abiria waliokaa mbele walirushwa na
kudondoka baharini.
Awali Ussi
aliwataka wamiliki wa vyombo vya baharini vya aina mbali mbali kuchukua kila
aina ya tahadhari zaidi katika kipindi hiki ambapo hali ya bahari imechafuka na
kuibuka kwa mawimbi makubwa.
Familia mia
mbili Wakati huo huo, zaidi ya familia mia mbili hazina makazi ya kuishi baada
ya nyumba 24 kuteketea kwa moto huko Shumba mjini katika Wilaya ya Micheweni
Mkoa wa Kaskazini Unguja. Mkuu wa Mkoa huo, Dadi Faki Dadi alithibitisha
kutokea kwa moto huo ambao chanzo chake kinasadikiwa kuwa, watoto walikuwa
wakipika chakula.
Dadi alisema
nyumba 14 zimeteketea moja kwa moja na moto huo, huku nyingine 10 zikiezuliwa
mapaa yake na wananchi kwa ajili ya kuchukua tahadhari ili moto usisababishe
madhara zaidi.
Makamo wa Pili
wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi alifika kuwapa pole wananchi wa kijiji hicho
ambao wamepata mkasa wa nyumba zao kuteketea kwa moto.
Alisema kazi
inayofanywa kwa sasa na Idara ya Maafa ni kufanya tathmini ya nyumba zote na
hasara hiyo kwa ajili ya kutoa fidia ili wananchi warudi katika makazi mapya.
No comments:
Post a Comment