MUUNDO wa serikali tatu uliomo ndani ya Rasimu ya Katiba iliyokabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete mwanzoni mwa wiki hii, umezua hofu kwa baadhi ya viongozi wa dini nchini, wakisema huenda ukachangia kuvunjika kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliodumu kwa miaka 50 sasa.
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo |
Aidha, mawazo ya kutaka serikali tatu yameelezwa yanatokana na watu kutokuwa na upendo wa kutosha na hofu ya Mungu.
Hayo yalisemwa jana na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wakati wa ufunguzi wa ibada ya misa ya shukrani, iliyoandaliwa na Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Alisema wanaolalamika juu ya muungano wa sasa wana yao, kwa kuwa unawazuia kufanya mambo yao wenyewe na kuingia mikataba kwa manufaa yao wenyewe.
“Kutokana na kuona kuwa wenzao ni kuzuizi, wanalalamika kwa kuwa Muungano unawazuia watu kuingia mikataba kama ya OIC (Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu). Sidhani kama huu ni umoja,” alisema Pengo na kuongeza kuwa, “Hofu yangu kubwa ni kwamba, kuwa na serikali tatu ndio mwisho wa Muungano. Tuombe ili tufikie malengo ya umoja.”
Alisema inapofikia hatua ya watu kuwaona wenzao kama ni mzigo na kutaka kujitenga haipendezi hata machoni pa Mwenyezi Mungu, badala yake wanapaswa kukaa na kuzungumza ili kujenga umoja thabiti, badala ya kufikiria kujitenga.
Hata hivyo alitoa mwito kwa wanasiasa na wananchi wote kuombea upendano na umoja katika vyama vya siasa ili vifikie maamuzi yaliyosahihi ya haki na yenye kujenga taifa.
Alisema ubinafsi ndio unaochochea mifarakano katika vyama; na watu kujitokeza tu kujitangaza uongozi bila chama husika kukubaliana hali inakuwa mbaya zaidi.
“Kamati za chama zikae kwa haki, ziseme zinamteua nani kwa sifa alizonazo kugombea nafasi fulani la hasha mtu mmoja anajitokeza na kuanza kusema anagombea nafasi fulani bila matakwa ya chama matokeo yake yanakuwa mabaya sana,” alisema Pengo.
Katika misa hiyo iliyoongozwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Titus Mdoe, WAWATA walitoa matoleo kwa wagonjwa walioko Taasisi ya Saratani ya Ocean Road yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni nane.
Askofu Titus Mdoe |
“Mama uwe mstari wa mbele kutimiza wajibu wako na kutenda yale ambayo ni haki kwa wote, na haki ya msingi kwa mtoto ni malezi mema. Mkishindwa kuwalea vema watalelewa na ibilisi na atawapa misingi ya kiibilisi, unatakiwa uwe mwakilishi mzuri sana wa Kristo popote ulipo, iwe kazini, mtaani, nyumbani au njiani,” alisema Askofu Mdoe.
Alisema katika kumshukuru Mungu kumaliza mwaka na kuwezesha kuanza mwaka mpya wapambane na changamoto walizozipata mwaka uliopita ili kuimarisha imani na umoja wao na pale walipoharibu wamwombe Mungu awaongoze na kuwatia nguvu.
No comments:
Post a Comment