Wizara ya Maliasili na Utalii
inapenda kuujulisha umma matokeo ya sensa ya tembo iliyofanyika mwezi Oktoba na
Novemba mwaka huu ili kuiwezesha Serikali kutambua hali ya rasilimali ya
wanyamapori ndani na nje ya maeneo yaliyohifadhiwa.
Wizara kwa kushirikiana na wataalamu wa ndani na
nje ya nchi imefanya sensa katika Maeneo ya Mfumo ikolojia wa Selous – Mikumi
na Ruaha – Rungwa pekee kwa kuwa ni maeneo yenye tembo wengi nchini.
Matokeo ya sensa hii yanaonyesha kwamba Mfumo wa
ikolojia wa Selous-Mikumi kwa sasa una tembo wapatao 13,084 na Ruaha–Rungwa una
tembo wapatao 20,090. Takwimu hizi zinaonesha kupungua kwa idadi ya tembo na
hasa katika mfumo ikolojia wa Selous-Mikumi ikilinganishwa na Sensa za awali.
Takwimu za muda mrefu zinaonesha kwamba mwaka
1976 katika mfumo ikolojia wa Selous–Mikumi kulikuwa na tembo 109,419. Idadi
hii ilipungua kufikia 22,208 mwaka 1991 kutokana na wimbi la ujangili
uliokuwepo katika kipindi cha mwaka 1984 -1989. Hata hivyo, idadi hiyo
iliongezeka na kufikia 70,406 mwaka 2006 baada ya Operesheni Uhai iliyofanyika
mwaka 1989 na 1990 na juhudi za kimataifa za uhifadhi ikiwemo kusitisha
biashara ya meno ya tembo.
Aidha, idadi ya tembo nchini ilipungua hadi
kufikia jumla ya tembo 38,975 mwaka 2009 na kuendelea kupungua hadi kufikia
tembo 13,084 hivi sasa.
Hali kama hiyo inaonekana pia katika mfumo wa
ikolojia wa Ruaha-Rungwa ambapo sensa ya mwaka 1990 ilionesha kuwa na tembo
11,712 kutokana na wimbi la ujangili. Idadi hii iliongezeka na kufikia 35,461
mwaka 2006. Hata hivyo, idadi hiyo imepungua na kubakia tembo 20,090 hivi sasa.
Kwa matokeo haya inaonesha kuwa katika mfumo
ikolojia wa Selous-Mikumi idadi ya tembo imepungua kwa asilimia 66
ikilinganishwa na idadi ya mwaka 2009 ambapo kulikuwa na jumla ya tembo 38,975.
na katika Mfumo ikolojia wa Ruaha–Rungwa Tembo wamepungua kwa asilimia 36.5
ikilinganishwa na idadi ya mwaka 2009 ambapo kulikuwa na jumla ya tembo wapatao
31,625.
Kupungua huku kunathibitishwa na idadi ya mizoga
ya tembo iliyohesabiwa wakati wa zoezi la sensa. Jumla ya mizoga 6,516 na 3,496
ilihesabiwa katika mifumo ikolojia ya Selous-Mikumi na Ruaha–Rungwa. Katika
zoezi hili Wizara ilitumia vigezo vya uwiano wa mizoga na tembo hai
waliohesabiwa (carcass ratio) kubaini vyanzo vya vifo hivyo. Katika hali ya
kawaida, uwiano wa asilimia 7 – 8 unaashiria vifo vya asili kama vile ugonjwa
na uzee. Zaidi ya asilimia hiyo inaashiria vifo visivyo vya asili.
Sensa iliyofanyika mwaka huu imeonesha uwiano wa
asilimia 30 kwa mfumo ikolojia wa Selous-Mikumi na asilimia 14.6 kwa
Ruaha–Rungwa. Kwa mujibu wa matokeo hayo, idadi kubwa ya vifo vya tembo
vimetokana na vifo visivyo vya asili.
Uchambuzi wa kina umebainisha kuwa asilimia 95 na
85 ya mizoga iliyoonekana katika mifumo ikolojia ya Selous-Mikumi na
Ruaha–Rungwa ni ya zaidi ya miezi 18 iliyopita.
Hii inaonesha kuwa juhudi za makusudi
zilizofanywa na serikali ikiwa ni pamoja na kuimarisha doria na operesheni
maalum mbalimbali za hivi karibuni zimesaidia kupunguza wimbi la ujangili kwa
kiasi kikubwa.
Aidha, kukamatwa kwa meno ya tembo yenye uzito wa
kilogramu 32,987 ndani na nje ya nchi katika kipindi cha 2008 hadi Septemba
2013 ni ishara tosha kuwa ujangili ni mojawapo ya sababu kubwa za kupungua kwa
idadi ya tembo nchini.
Sababu nyingine ni kuongezeka kwa mifugo katika
maeneo yaliyohifadhiwa na shoroba za wanyamapori. Mathalan, katika Pori Tengefu
la Kilombero ambalo ni sehemu ya ikolojia ya Selous – Mikumi, mwaka 2002
lilikuwa na tembo 2,080, katika sensa ya mwaka huu, hukukuwa na tembo hata
mmoja.
Ongezeko la bei katika masoko ya biashara haramu
ya meno ya tembo hususan katika nchi za Mashariki ya mbali ni kichocheo na
kisababishi kikubwa.
Kufuatia hali hii, Wizara inaimarisha ulinzi wa
wanyamapori kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na taasisi
nyingine za kanda na kimataifa pamoja na kuelimisha na kushirikisha wananchi
katika masuala mbalimbali ya uhifadhi.
Ili kuimarisha na kuboresha shughuli za uhifadhi,
Wizara iko katika hatua za mwisho za kuanzisha mamlaka mpya ya wanyamapori.
Vilevile sheria za uhifadhi zinapitiwa ili kuruhusu kuanzishwa kwa mfumo wa
kijeshi kwa watumishi wa sekta ya wanyamapori.
Wizara inapenda kuwatambua na kuwashukuru wafadhili
wote waliofanikisha sensa hii iliyogharimu kiasi cha dola za kimarekani
160,000ikiwa ni fedha za serikali na wafadhili. Wafadhili hao ni Shirika la
Misaada ya Kiufundi la Ujerumani (GIZ) kupitia Frankfurt Zoological Society
(FZS) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) kupitia Mradi wa
TANAPA wa SPANEST.
Imetolewa na
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii
Mhe. Lazaro Nyalandu (MB)
10/01/2014
No comments:
Post a Comment