
SERIKALI ya Uganda
tayari imeshaanza kulipa deni lake kwa Tanzania la dola za Marekani milioni 9.6
kati ya dola za Marekani milioni 18.4 ikiwa ni fidia kwa Tanzania kwa mchango
wake katika kumuondoa Idd Amin Dada Uganda mwaka 1978.
Hayo yalibainishwa
bungeni jana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Shamsi Vuai
Nahodha, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mbinga, John Komba (CCM).
Katika swali lake
Komba alitaka kujua kama Tanzania ilishaanza kudai fidia kwa Serikali ya Uganda
kutokana na mchango wake wa kuisaidia nchi hiyo kumuondoa Idd Amin na kumfanya
Rais wa sasa Yoweri Museveni kutawala kwa amani nchini humo.
Akijibu swali hilo,
Nahodha alikiri kuwa Tanzania ilipigana vita na Uganda kuanzia mwaka 1978 hadi
mwaka 1979 kutokana na uvamizi uliofanywa na Uganda chini ya utawala wa Idd
Amin aliyevamia na kukalia sehemu ya ardhi ya Tanzania mkoani Kagera.
“Kwa kuwa vita hivyo
vilitokana na uvamizi wa Idd Amin, baada ya vita kumalizika Serikali ya
Tanzania iliitaka Uganda kulipa fidia. Serikali hiyo nayo ilikubali kuilipa
Tanzania fidia hiyo,” alisema Nahodha.
Alisema kwa bahati
mbaya Serikali ya Uganda haikutekeleza makubaliano hayo yaliyofanyika mwaka
1979 hivyo Serikali ya awamu ya tatu ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais
Mstaafuma William Benjamin Mkapa ilifanya majadiliano tena na Uganda.
Alisema kutokana na
majadiliano hayo Serikali ya Uganda ilitakiwa kulipa fidia dola za Marekani
milioni 18.4 na hadi sasa Serikali hiyo imeshalipa dola za Marekani milioni 9.6
fedha ambazo ziliwekwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali na nchi hiyo kubakiwa na
deni la dola za Marekani milioni 8.8.
Nahodha alisema
majadiliano baina ya Tanzania na Uganda yanaendelea ili sehemu ya fidia
iliyobaki iweze kulipwa chini ya Wizara ya Fedha ambayo ndio inayofuatilia deni
hilo.
Akijibu swali la
nyongeza la Komba la kuitaka Tanzania imkumbushe Museveni juu ya namna Tanzania
ilivyosaidia nchi yake hivyo aache kuihujumu kwa kusaidiana na Rais wa Rwanda
Paul Kagame, Nahodha alisema siku zote Tanzania haimsaidii mtu ili kupata
shukurani. “
Tanzania ni nchi ya
kipekee sana, imebahatika kupata viongozi wenye sifa kubwa duniani kama Nyerere
(Mwalimu Julius), kiongozi huyu aliwahi kusema Waafrika ni ndugu na Afrika yetu
sote, tuliwasaidia Uganda kwa utu hatutegemei zaidi,” alisisitiza.
Alisema hata juzi
baada ya kifo cha Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Tanzania
ilitoa tamko la kumuenzi kwa kusisitiza uvumilivu, jambo ambalo limeipatia sifa
kubwa Tanzania. “Naomba tuendelee kuitunza sifa hii na si vinginevyo.”
No comments:
Post a Comment