![]() |
| Zitto Kabwe |
MGOGORO wa uongozi
ndani ya Chadema, sasa umehamishiwa rasmi Baraza Kuu kwenye mpasuko, baada ya
watuhumiwa waliovuliwa madaraka na Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, kukata rufaa
huko wakijua kuna wapinzani waliojitokeza hadharani dhidi ya CC na Mwenyekiti
Freeman Mbowe.
CC ya Chadema,
iliwavua madaraka Naibu Katibu Mkuu na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe, Mjumbe wa CC, Dk Kitila Mkumbo na Mwenyekiti wa
Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Chama hicho kilidai
kuwa hatua hiyo ilitokana na usaliti na njama za kutaka kufanya mapinduzi, huku
wenyewe wakijitetea hadharani kuwa walitaka kumtumia Zitto, agombee uenyekiti
wa Taifa dhidi ya Mbowe, ambaye anatajwa kutaka kuutetea. Jana mwanasheria wa
watuhumiwa hao, Albert Msando, alitangaza hatua iliyochukuliwa na viongozi hao,
kwamba ni kupinga uamuzi wa CC kwa Baraza Kuu.
“Kuna sababu mbili
za msingi za kukata rufaa; kwanza utaratibu wa kuchukua hatua za nidhamu
ulikiukwa, na pili, sababu za kuchukuliwa hatua hizo si sahihi,” alisema
Msando, ambaye alipata kuwa wakili wa Mbowe. Moto Baraza Kuu Hatua ya akina
Zitto ilitarajiwa na wengi kwa kuwa baada ya uamuzi huo wa Kamati Kuu, Dk
Mkumbo, ambaye ndiye aliyeandika Ilani ya Uchaguzi ya Chadema, alikubaliana nao
lakini aliukosoa.
“Kwa mujibu wa
Katiba ya Chadema, Sura ya Sita, Ibara ya 6.3.6 (b); ‘kiongozi aliyeteuliwa na
vikao vya juu vya uongozi atasimamishwa au kuachishwa uongozi na kikao
kilichomteua.
“Mimi nilichaguliwa
na Baraza Kuu na ni kikao hiki pekee chenye uwezo wa kunivua nafasi niliyonayo.
Ninaamini wajumbe wa CC walipitiwa katika hili, kwa sababu siamini kwamba
hawajui matakwa haya ya kikatiba, ukizingatia kwamba ndani yake kuna wajumbe
waliobobea kabisa katika tasnia ya sheria,” alisema.
Mbali na kauli hiyo
ya Dk Mkumbo, msomi ambaye alikuwa pia mwandishi wa hotuba za mgombea urais wa
Chadema mwaka 2010, Dk Willibrod Slaa, baadhi ya wajumbe wa Baraza walijitoa
mhanga kumwunga mkono Zitto na kuipinga CC hadharani, huku wakimtaka Mbowe
aitishe kikao cha dharura cha Baraza Kuu.
Kanda ya Dar es
Salaam Mjumbe wa kwanza kufanya hivyo, alikuwa Patrick Joseph, Mjumbe wa Baraza
Kuu pamoja na vyeo vingine, ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Baraza la Vijana
la Taifa (Bavicha).
“Nimefadhaishwa
sana na uamuzi uliofikiwa na CC ya chama dhidi ya Zitto na Dk Mkumbo mbali na
kwamba CC haikuwa na mamlaka ya kikanuni wala kikatiba kufikia uamuzi
ilioufikia na kuutangaza kwa umma.
“Msimamo wangu,
namtaka Mwenyekiti (Mbowe) akishirikiana na watendaji wengine wa chama waitishe
mkutano wa dharura wa Baraza Kuu, ili tutoe uamuzi sahihi wa suala hili.
“Ninataka pia
pamoja na ajenda zitakazojadiliwa, watueleze ni kwa nini tusiamini kwamba
uamuzi huu umeathiriwa na hofu ya uchaguzi ndani ya chama. Ni kitu gani
kimeifanya Sekretarieti ya CC itangaze ratiba ya Uchaguzi Mkuu baada ya
kuchafua watu waliotarajiwa kugombea nafasi mbali mbali mpaka kuwavua
uanachama?” alihoji Joseph.
Kanda ya Kusini
Wajumbe wengine kujitoa mhanga ni Ally Chitanda, aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa
wa Lindi, Kanda ya Kusini na Katibu wa Sekretarieti ya CC. Katika taarifa yake,
alisema:
“Ningependa
kuwaambia wana Chadema na Watanzania kwa ujumla, uamuzi huu wa Kamati Kuu wa
kuwavua uongozi Zitto na Dk Mkumbo ni wa kijuha na unaofanya Watanzania sasa
waangalie mara mbili mbili kama hawa watu wako makini na huo ukombozi wanaousema.”
Kanda ya Kati,
Kigoma Kutoka Kanda ya Kati, Mjumbe wa Baraza Kuu na aliyekuwa Mwenyekiti wa
Mkoa, Wilfred Kitundu alijiuzulu nafasi yake na kubaki na ujumbe wa Baraza.
“Tunalaani, kupinga
na kukemea CC ya chama dhidi ya uamuzi wao huu uliojaa chuki, hofu na wasiwasi
mwingi kuelekea uchaguzi mkuu ndani ya chama.
“Tunamtaka
Mwenyekiti na Katibu Mkuu, waitishe mara moja mkutano wa Baraza Kuu la chama
kutolea uamuzi suala hilo. Kigoma, Mjumbe wa Baraza Kuu na Mwenyekiti wa Mkoa,
Jafari Kasisiko, alisema:
“Maoni ya wengi
mkoani na viongozi wa chama ni kuudhiwa na uamuzi ya CC ambao dhahiri ulilenga
kummaliza Zitto kisiasa.” Kwa Msajili Mbali na kukata rufaa Baraza Kuu,
Mwigamba alikwenda mbali zaidi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis
Mutungi, kushitaki alichoita ni kuchezewa kwa Katiba ya Chama.
“Nitaomba (Msajili)
atoe mwongozo kuhusu mgogoro wa kikatiba ndani ya chama unaotokana na kipengele
cha Katiba kinachogusia ukomo wa uongozi kubadilishwa kinyume na utaratibu,”
alisema Mwigamba. Mwigamba anadai kuwa Katiba ya 2004, kipengele 5.3.2 (c)
kinachosomeka:
“Muda wa Uongozi:
Kiongozi aliyemaliza muda wa uongozi, ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena,
ili mradi awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi kwa muda usiozidi
vipindi viwili katika cheo kimoja kwa ngazi moja. Katiba ya sasa ya mwaka 2006,
kipengele cha 6.3.2 ( c) kinachozungumzia muda wa uongozi kinasomeka: “Kiongozi
aliyemaliza muda wa ungozi, ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena, ili mradi
awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi.”
Mwigamba anadai
maneno ‘kwa muda usiozidi vipindi viwili katika cheo kimoja kwa ngazi moja’,
yaliondolewa kinyemela wakati wa kuchapisha Katiba hiyo.
Anakiri ni kweli
kuwa marekebisho ya Katiba yalifanyika mwaka 2006, lakini hoja ya kubadili
kipengele hicho haikuwapo na mihutasari inaonesha wazi hakukuwa na mjadala wa
kipengele hicho au kuhusu suala zima la ukomo wa uongozi.
Kama hoja hiyo
ikipita na kukubaliwa na Msajili, Mbowe atakuwa amepoteza haki ya kutetea
nafasi yake kama Mwenyekiti wa Taifa, kwa kuwa ameshaongoza kwa vipindi viwili
na kumpa nafasi Zitto ambaye alishaonesha nia siku nyingi ya kuitaka nafasi
hiyo.
Kama hoja hiyo
ikikosa mashiko kwa Msajili, Mbowe atakuwa na fursa ya kutetea kiti hicho kwa
mara ya tatu, na atakuwa Mwenyekiti wa kwanza kufanya hivyo kwa kuwa huko nyuma
Katiba haikuruhusu.
Chanzo ;

No comments:
Post a Comment