Polisi nchini Tanzania wamesema
shehena ya Pembe za Tembo zilizokamatwa katika bandari ya Zanzibar ni sawa na
Tembo mia tatu na watano, zikiwa na thamani ya karibu shilingi bilioni nane,
sawa na karibu dola milioni tano za Kimarekani.
Watu wawili wanashikiliwa na polisi
kwa tuhuma za kuhusika na pembe hizo, huku maafisa wawili wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania, TRA, na mmoja wa Mamlaka ya Bandari pia wamekamatwa kuhusiana na
tukio hilo.
Kwa mujibu wa afisa habari mkuu wa
jeshi la polisi Zanzibar, Inspekta Mohammed Mhina, watuhumiwa wa kesi hii
watafikishwa katika mahakama jijini Dar es Salaam.
Pembe hizo zilikuwa zimefichwa
kwenye kontena la urefu wa mita 40, tayari kwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Serikali ya Tanzania iko katika
kampeni kamambe ya kupambana na ujangili ili kunusuru wanyama pori ambao wako
hatari kutoweka kutoka na kushamiri kwa biashara ya meno ya tembo na vipusa vya
faru.
Iliripotiwa kuwa wastani wa tembo 30
huuawa kila siku nchini Tanzania, hali iliyoilazimisha serikali kukabiliana na
mtandao wa ujangili, ambao unatuhumiwa kuunganisha watu wa kada mbalimbali,
wakiwemo wawindaji, wasafirishaji na wafanyabiashara wakubwa ndani na nje ya
nchi.
Hivi karibuni raia watatu wa China
walikamatwa nchini Tanzania kwa kukutwa na pembe 706 ya tembo, sawa na Tembo
353 waliouawa katika hifadhi mbalimbali nchini humo.

No comments:
Post a Comment