
MVUTANO unaoashiria
mapigano na mauaji kwa mara nyingine tena unafukuta baina ya wakulima na
wafugaji Wilayani Kilindi Mkoani Tanga baada ya wafugaji kuchoshwa na
matukio ya kikatili ya mifugo yao kuuawa kwa kuwekewa
sumu kwenye malisho na kufia porini.
Tukio hilo la kusikitisha
lilitokea juzi katika kitongoji cha Kipaluke, Kijiji cha Kigwama, Kata ya
Msanja Tarafa ya Mswaki Wilayani Kilindi ambako ng'ombe nane
walifia porini kati ya 14 waliyodaiwa kula majani yenye sumu.
Wakizungumzia tukio hilo la
kinyama, jamii ya wafugaji walilalamikia kuchoshwa na maisha ya kunyanyaswa na
kufanyiwa vitendo vya ukiukwaji wa haki na wakulima ambao wanalindwa na
kupewa baraka na baadhi ya viongozi.
Wilaya ya Kilindi imekuwa ikikabiliwa
na machafuko ya mara kwa mara na kusababisha vifo na majeruhi kwa kile
kilichokuwa kikielezwa kuwa ni viongozi kutokuwa na tahadhari ya kushughulikia
migogoro mapema hadi yanapotokea maafa.
Wakizungumza katika mkutano wa dharula
wa wafugaji hao wa jamii ya kimasai uliyofanyika jana katika kitongoji cha
Kipaluke,wafugaji hao wakiongozwa na Philipo Ngakuru mwenyekiti wa
serikali ya kitongoji cha Kipaluke na Marko Issaya kiongozi wa
kijadi wa jamii hiyo (Raigwanani), walisema hali ilipofikia
watalazimika kuingia msituni kufanya vita.
katika mkutano huo viongozi hao
walichukua jukumu la kuzuia machafuko hayo wakiaahidi jamii hiyo kwamba
watafuatilia ngazi za juu za serikali ili kupatiwa ufumbuzi wa
matukio hayo na hatimaye haki itendeke kwa njia ya amani ambayo ni
utamaduni wa taifa letu.
Wakati wakizungumza kwenye
mkutano huo walidai kuwa tatizo lao na wakulima linastawishwa na vyombo husika
kushindwa kusimamia makubaliano ya kisheria juu ya matumizi halali ya eneo
lenye mgogoro na kwamba hata pale wanapoomba serikali kuingilia kati hakuna
kinachotendeka.
Naye Thomas Tinno aliitaka serikali
kutokaa kimya na badala yake itoe tamko kuhusiana na kitendo cha kumwagwa sugu
kwenye malisho ya wanyama na kusababisha vifo na kueleza kuwa kufanya
hivyo kutazuia maamuzi ya hasira ya kulipa kisasi yanayoweza kuchukuliwa
na wahanga.
“Mimi naiomba serikali kupitia nyinyi
waandishi wa habari ichukue hatua kwani waliyohusika na tukio hili wanafahamika
isingoje wahanga wachukue hatua, kwani kukaa kimya itakuwa imebariki machafuko”
alisema Tinno.
Abraham Ngakuru alisema kuwa
kutokana na tukio hili, jamii ya wafugaji imetangaza mgogoro na kwamba kama si
busara za viongozi wao wa kijadi amani ingetoweka tangu pale serikali
ilipojidhihirisha kusimama na kutetea upande mmoja wa wakulima hao.
Aidha Paulo Sinion alidai kuwa
siku ya tukio majira ya saa tisa jioni walipata taarifa kutoka kwa
mchungaji kuwa ng’ombe zinaanguka na walipofika walizikuta 14 zikigaagaa
chini na kwamba sita zilinusurika kufa baada ya kupewa maziwa na sukari ambapo
nane kati ya hizo zilikufa hapohapo.
Akitoa tamko la mkutano huo,
Philipo ambaye ni mwenyekiti wa serikali ya Kitongoji hicho, alisema kuwa
tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji limekuwa sugu na kueleza bayana kuwa
unachochewa na uongozi wa Kata na baadhi ya serikali za vijiji.
Kwamujibu wa Philipo ni kuwa
viongozi wa Kata kwa kushirikiana na wa vijiji wamekuwa na utamaduni wa
kuwanyanyasa wafugaji kwa vitendo mbalimbali kama vile kuunda kikundi cha
vijana kwa ajili ya kuhujumu mifugo yao.
Alisema kuwa kutokana na hali ilivyo
ni lazima serikali ya Wilaya na Mkoa iingilie kati kukomesha unyanyasaji huo
unaofanywa kwa lengo la kuwanufaisha wachache ili kuzuia vurugu zinazoweza
kutokea katika maeneo hayo.
Alishangaa uongozi wa Kata
kutolishughulikia tatizo hilo kwa madai kuwa lipo wazi kwani sehemu yenye
mgogoro inayotumiwa kwa ufugaji ilitengwa na serikali tangu mwaka
1998 kuwa eneo la malisho na kuhoji sababu za kutoheshimiwa.
Kiongozi wa jamii hiyo, Raigwanani
Issaya yeye alikitaka Chama cha Mapinduzim CCM kuingilia kati mgogoro huo kwani
wafugaji hao wananyanyashwa na watendaji wake na hawapati
haki licha ya kuwa ni wafuasi wa Chama hicho.
Aidha alienda mbali zaidi kwa kukitaka
Chama hicho kumshauri Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Kilindi kumuondoa
afisa mtendaji wa Kata ya Msanja akieleza kuwa ni mzigo na chanzo cha
unyanyasaji ndani ya Kata hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Seleman
Liwowa alidai hakuwa na taarifa ya tukio hilo na kuahidi kufuatilia ili
kubaini na kuchukua hatua zinazostahili na kwamba ni kosa la jinai kwa mtu
kutumia vibaya madaraka yake jambo ambalo pia ni kinyume na uwepo wa kiongozi
husika.
“Hapana Mimi sina taarifa hizo
ndiyo unanambia sasa hivi, japo kuwa sipo Wilayani, nipo Mtwara…..nitawasiliana
na (OCD) Mkuu wa polisi Wilaya afuatilie kwa kuwa wewe unanieleza tofauti na
taarifa nilizokuwa nazo” Liwowa alisema.
No comments:
Post a Comment