
Na Oscar Assenga, Tanga
SIKU Chache baada ya Kamati kuu ya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo Taifa (Chadema) kuamua kumvua uongozi ndani
ya chama hicho aliyekuwa katibu Msaidizi Zitto Kabwe chama hicho mkoani hapa
kimeipongeza hatua hiyo kwa kusema italeta umakini mkubwa kwa viongozi
waliobaki.
Uamuzi huo ulitolewa kwa mujibu ibara
ya 7.7.16 kifungu (V) ambayo inaeleza kuwa kamati hiyo ina mamlaka ya
kumwachisha ujumbe wa kamati kuu mjumbe mteule ambaye ataenda kinyume cha
katiba, kanuni na maadili au kushindwa kukidhi matakwa ya kuteuliwa kwake.
Akizungumza na Tanga Raha,Katibu wa
Chadema Mkoa wa Tanga,Jonathan Bahweje alisema suala hilo lilipaswa kufanywa na
kamati hiyo kwa sababu ni sahihi kwa mtu yoyote anayekiuka kanuni na taratibu
za uongozi ndani ya chama hicho.
Bahweje alisema hatua ya Zitto kukiri
kuwa alikosea na kupewa adhabu ya siku kumi na nne kujitetea kwa kamati kuu ya
chama hicho alitumia busara kubwa sana na kuwataka wanachama kuwa na utulivu
wakati mchakato huo ukiendelea.
“Maamuzi ya kamati kuu
yaliyofanywa sidhani kama yanaweza kuingiliwa na upande mwengine hivyo napenda
kuwaasa viongozi wa ngazi za chini kuacha kuingilia suala hilo kwani tayari
limeshapata muafaka “Alisema Bahweje.
Alisema wanaiomba kamati kuu ya chama
hicho kumaliza mgogoro uliopo huo mapema ili kuweza kujiandaa na uchaguzi mkuu
wa serikali za mitaa mwaka 2014 kwani wamedhamiri kuhakikisha wanashinda
katika chaguzi hizo.
Katibu huyo aliitaka kamati hiyo
kukemea viongozi ambao wanapiga maamuzi yao kwani wao ndio chombo cha mwisho
ambacho kinauwezo wa kufanya jambo lolote ambalo linaweza kuleta mgawanyiko
ndani ya chama hicho.
“Naishauri kamati kutumia
nafasi yao kuwaonya viongozi kuanzia ngazi za chini na kuweza kuleta mshikamano
wa pamoja ambao utaweza kuleta mafanikio katika chama chetu kwani uongozi imara
ndio utakiwezesha kuwatumikia wananchi “Alisema Bahweje
No comments:
Post a Comment