BODI YA LIGI YAFUNGIA VIWANJA SABA.
BODI
ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) imefungia viwanja saba vilivyokuwa vikitumiwa
na timu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) hadi
vitakapofanyiwa marekebisho ili kukidhi mahitaji ya mechi za mpira wa
miguu.
Uamuzi
huo umefikiwa na TPL Board katika kikao chake cha kwanza kilichofanyika juzi
(Novemba 10 mwaka huu) jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine
kilipitia ripoti za mechi za VPL na FDL katika mzunguko wa kwanza.
Viwanja
vilivyofungiwa na marekebisho yanayotakiwa kufanyika kwanza ili viruhusiwe
kutumika tena ni Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba (majukwaa yake yamechakaa,
hivyo kuhatarisha usalama wa watazamaji), na Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini
Tanga (vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo (dressing rooms) havina
hadhi).
Uwanja
wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya (sehemu ya kuchezea- pitch ni mbovu),
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha (pitch ni
mbovu), Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi (vyumba vya kubadilishia kutumika kwa ajili
ya shule ya awali), Uwanja wa Majimaji mjini Songea (pitch ni mbovu) na Uwanja
wa Jamhuri mjini Morogoro (pitch ni mbovu).
Klabu
ambazo timu zake zinatumia viwanja hivyo zimeshaarifiwa rasmi juu ya uamuzi huo
ambapo ama vinatakiwa kuwasiliana na wamiliki wa viwanja hivyo ili wafanye
marekebisho au kutafuta viwanja vingine vya kuchezea mechi zao. Kwa upande
wa ripoti za mechi za VPL; Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 na kupewa
onyo kali kwa timu yake ya U20 kutocheza mechi ya utangulizi walipocheza na
Yanga.
Pia
wanatakiwa kulipa gharama za uharibifu baada ya washabiki wao kuvunja kioo cha
basi la Yanga baada ya gharama hizo kuthibitishwa na Bodi ya Ligi. Pia
Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa washabiki wake kushambulia basi la
wachezaji wa Tanzania Prisons baada ya mechi dhidi yao, na kulipa gharama za
uharibifu baada ya kuthibitisha na Bodi ya Ligi. Coastal Union imepigwa
faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake ilipocheza na Azam
kwenye Uwanja wa Mkwakwani ambapo mwamuzi msaidizi Hassan Zani alishambuliwa
kwa mawe na kujeruhiwa mkononi na kichwa, tukio lililosababisha mchezo kusimama
kwa dakika tatu.
Beki
wa Coastal Union, Hamad Khamis wa Coastal Union amepigwa faini ya sh. 500,000
kwa kumpiga kichwa kwa makusudi Kipre Tchetche wa Azam. Kitendo hicho
kilisababisha refa amtoe nje kwa kadi nyekundu, hivyo atakosa mechi tatu
zinazofuata za timu yake.
Mchezaji
Cosmas Lewis wa Ruvu Shooting alifanya kitendo cha utovu wa nidhamu kwa kupiga
kelele wakati mgeni rasmi akisalimia timu na kukataa kupeana mkono na kamishna
kwenye mechi dhidi ya Rhino Rangers, hivyo amefungiwa mechi tatu na kupigwa
faini ya sh. 500,000.
Mtunza
vifaa (Kit Man) wa JKT Ruvu, Selemani Oga aliondolewa kwenye benchi la ufundi
wakati wa mechi yao dhidi ya Mbeya City kwa kosa la kutoa lugha chafu kwa refa,
hivyo suala lake litapelekwa katika Kamati ya Maadili.
Kocha
Msaidizi wa Oljoro JKT, Fikiri Elias amepigwa faini ya sh. 500,000 na kufungiwa
mechi tatu kwa kumshambulia kwa matusi refa wakati wa mechi yao dhidi ya
Ashanti United. Naye mtunza vifaa wa timu hiyo Elas Justin amepelekwa Kamati ya
Maadili kwa kumshambulia refa kwa matusi ya nguoni.
Simba
wamepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake wakati wa
mechi dhidi ya Kagera Sugar. Katika FDL, mchezaji Ally Mtoni wa Villa
Squad amepigwa faini y ash. 200,000 na kufungiwa mechi tano. Kosa lake ni
kujisaidia haja ndogo golini wakti wa mechi dhidi ya Ndanda FC iliyochezwa mjini
Mtwara. Kamishna Paul Opiyo wa mechi ya FDL kati ya Villa Squad na Transit
Camp kwa kutokuwa makini.
Katika
ripoti yake ameeleza kuwa Transit Camp ilichelewa kufika uwanjani, lakini
hakusema ilichelewa kwa muda gani. Kocha wa Polisi Dar es Salaam, Ngelo
Nyanjabha na Meneja wa timu hiyo Mrimi Masi wamepigwa faini ya sh. 200,000 na
kufungiwa mechi tatu kila mmoja kwa kuongoza kundi la washabiki kumvamia refa
wa mechi yao dhidi ya Villa Squad iliyochezwa Dar es Salaam.
Pia
Bodi ya Ligi imeagiza Polisi waandikiwe barua ya onyo kwa vile wakati waamuzi
wanapigwa walikuwepo lakini hawakutoa msaada kwa wakati. Kocha wa Friends
Rangers, Kheri Mzozo amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi sita kwa
kosa la kumtukana refa na kutishia kuhamamisha washabiki waingie uwanjani
kufanya fujo kwenye mechi dhidi ya Villa Squad.
Naye
Kocha msaidizi wa timu ya Transit Camp, Haji Amiri amepigwa faini ya sh.
200,000 na kufungiwa mechi sita kwa kutoa lugha ya matusi kwa mwamuzi wa akida
wakati wa mechi dhidi ya Friends Rangers. Adhabu zote zimetolewa kwa
mujibu wa kanuni. Pia Bodi ya Ligi imeahirisha kufanya uamuzi wa mechi kati ya
Stand United na Kanembwa JKT iliyochezwa Uwanja wa Kambarage ili kukusanya
taarifa zaidi. Mechi hiyo haikumalizika. Bodi ya Ligi itakutana tena Jumapili
(Novemba 17 mwaka huu).

No comments:
Post a Comment