UHAI
CUP KUANZA KUTIMUA VUMBI NOV 17
Michuano ya Kombe la Uhai
inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 wa klabu za Ligi Kuu
inaanza kutimua vumbi Novemba 17 mwaka huu katika viwanja vya Karume na Azam
Complex, Dar es Salaam.
Droo ya michuano hiyo inayodhaminiwa na
Maji Uhai imefanyika leo (Novemba 8 mwaka huu) mbele ya waandishi wa habari
katika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambapo timu
zimepangwa katika makundi matatu.
Kundi A linaundwa na timu za Azam,
Coastal Union, JKT Ruvu Stars, Mbeya City na Yanga, wakati kundi B ni Ashanti
United, Mgambo Shooting, Oljoro JKT na Ruvu Shooting. Kagera Sugar, Mtibwa
Sugar, Rhino Rangers na Tanzania Prisons ndizo zinazounda kundi C.
Mechi za ufunguzi kundi A Novemba 17
mwaka huu ni kati ya Azam na Coastal Union (saa 2 asubuhi- Karume), Yanga na
Mbeya City (saa 8 mchana- Karume). Kundi B ni Ruvu Shooting na Ashanti United
(saa 4 asubuhi- Karume), Oljoro JKT na Simba (saa 10 jioni- Karume).
Kagera Sugar na Mtibwa Sugar (saa 2
asubuhi- Azam) na Rhino Rangers na Tanzania Prisons (saa 10 jioni- Azam) ndizo
zitakazocheza mechi za ufunguzi Novemba 17 mwaka huu katika kundi C.
Robo fainali ya michuano hiyo itachezwa
Novemba 24 na 25 mwaka huu wakati nusu fainali itapigwa Novemba 26 na 27 mwaka
huu. Mechi ya kutafuta mshindi wa tatu na ile ya fainali zitachezwa Novemba 30
mwaka.
TANZANITE
YATUA SALAMA MAPUTO
Kikosi cha timu ya Taifa ya wanawake
chini ya miaka 20 (Tanzanite) kimewasili salama jijini Maputo, Msumbiji tayari
kwa mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza ya Kombe la Dunia itakayochezwa
kesho (Novemba 9 mwaka huu).
Kwa mujibu wa kiongozi wa msafara wa
Tanzanite, Kidao Wilfred ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), timu hiyo chini ya Kocha wake
Rogasian Kaijage ilifanya mazoezi yake ya kwanza jana asubuhi.
Tanzanite itafanya mazoezi yake ya
mwisho leo (Novemba 8 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa wa Zimpeto ambao ndiyo
utakaotumika kwa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni kwa saa
za Msumbiji.
Nao wachezaji waliobaki kumalizia
mtihani yao ya kidato cha nne wameondoka leo saa 11 jioni kwa ndege ya LAM
wakiongozwa na naibu kiongozi wa msafara, Khadija Abdallah Nuhu ambaye ni
mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA).
KESSY
KUSIMAMIA MECHI YA KOMBE LA DUNIA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) limemteua Lina Kessy kuwa kamishna wa mechi ya Kombe la Dunia Kanda ya
Afrika kwa wanawake chini ya umri wa miaka 20 kati ya Afrika Kusini na
Botswana.
Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya
kwanza itachezwa nchini Afrika Kusini, Novemba 9 mwaka huu. Waamuzi kutoka
Zambia ndiyo watakaochezesha mechi hiyo namba kumi.
Waamuzi hao wataongozwa na Glads lengwe
atakayepuliza filimbi wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Bernadette Kwimbira
kutoka Malawi, namba mbili ni Mercy Zulu na mezani atakuwepo Sarah Ramadhani,
wote wa Zambia.
Afrika Kusini ilishinda mechi ya kwanza
ugenini mabao 5-2. Mshindi wa mechi hiyo atacheza raundi ya pili na mshindi wa
mechi kati ya Tanzania na Msumbiji.
MECHI
YA JKT RUVU, COASTAL YAINGIZA LAKI 2/-
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati
ya wenyeji JKT Ruvu na Coastal Union ya Tanga iliyochezwa juzi (Novemba 6 mwaka
huu) Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam imeingiza sh. 201,000.
JKT Ruvu iliibuka na ushindi wa bao 1-0
katika mechi hiyo namba 85 na kushuhudiwa na watazamaji 67 waliokata tiketi kwa
viingilio vya sh. 3,000 na 10,000.
Kila klabu ilipata mgawo wa sh. 39,010
wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 30,661.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni
asilimia 15 ya uwanja sh. 19,835, tiketi sh. 38,100, gharama za mechi sh.
11,901, Bodi ya Ligi sh. 11,901, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh.
5,950 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 4,628.
Nayo mechi kati ya Ashanti United na
Simba iliyochezwa juzi Uwanja wa Taifa imeingiza(Mil 24) sh. 24,931,000 ambapo
kila klabu ilipata mgawo wa sh. 5,333,590.
Wakati huo huo, mechi za jana (Novemba
7 mwaka huu) kati ya Yanga na Oljoro imeingiza(Mil 34) sh. 34,902,000 kutokana
na watazamaji 6,045 ambapo kila klabu imepata sh. 7,812,477.95. Mechi ya Azam
na Mbeya City iliyochezwa Azam Complex yenyewe imeingiza sh. 15,973,000 kwa
watazamaji 4,857 na kila klabu imepata sh. 3,953,162.
WATATU
WAOMBEWA ITC KUCHEZA UJERUMANI
Watanzania watatu wameombewa Hati ya
Uhamisho wa Kimataifa (ITC) na Chama cha Mpira wa Miguu Ujerumani (DFB) ili
wacheze mpira wa miguu nchini humo.
Wachezaji hao ni Charles Mishetto na
David Sondo wanaombewa hati hiyo ili waweze kujiunga na timu ya SpVgg 1914
Selbitz, wakati Eric Magesa ameombewa kibali hicho ili achezee timu ya klabu ya
SC Morslingen.
Hata hivyo, katika maombi hayo DFB
haikuleza hapa nchini walikuwa wakicheza katika klabu zipi. Wachezaji wote
wameombewa hati hiyo kama wachezaji wa ridhaa.
Boniface
Wambura Mgoyo
Kaimu
Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF)

No comments:
Post a Comment