MFUNGAJI bora wa mashindano ya Umoja na Amani, yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Ubungo Msewe, Dar es Salaam, James Msuva amesajiliwa timu ya vijana ya Simba SC, maarufu kama Simba B na tayari amejiunga nayo.
Mhitimu huyo
wa kidato cha Nne katika sekondari ya Makongo, Dar es Salaam aling’ara katika
mashindano hayo yaliyoandaliwa na Waziri a Habari, Utamaduni na Michezo, Dk
Fenella Mukangara akiichezea Baruti FC mwezi uliopita kwa kufunga mabao saba na
kuiwezesha timu yake ya mtaani kutwaa Kombe hilo.
James aliyekwenda Sapphire jana kumtembelea kaka yake, Simon Msuva wa Yanga SC aliye kambini na timu ya pili ya taifa, Future Young Taifa Stars, alisema kwamba anamshukuru Mungu anaendelea vizuri Simba B.
“Natarajia kuichezea Simba katika mashindano ya Kombe la Uhai (michuano maalum ya timu za vijana za Ligi Kuu) na nikipata nafasi hiyo itakuwa fursa nzuri kwangu kuzidi kupambanua kipaji changu,”alisema.
Msuva mdogo aliitwa na Waziri Mukangara ofisini kwake kwa lengo la kumsaidia zaidi kumuendeleza kisoka, baada ya kuonyesha kipaji kikubwa katika michuano ya Kombe la Umoja na Amani.
James
anayemfuatia Simon Msuva kuzaliwa, amehitimu Kidato cha Nne katika sekondari ya
Makongo, Dar es Salaam na pamoja na kuchezea Barudi FC kama timu ya mtaani, pia
alikuwa katika akademi ya Wakati ya Ujao, iliyoasisiwa na kocha wa zamani wa
Simba, Mholanzi Ronny Mintjens.
No comments:
Post a Comment